May 23, 2024 11:02 UTC
  • Kaimu Rais: Iran itaendelea kuunga mkono kambi ya muqawama

Kaimu Rais wa Iran amesema Jamhuri ya Kiislamu itaendelea kuunga mkono kikamilifu kambi ya muqawama.

Mohammad Mokhber, Kaimu Rais wa Iran amesema hayo leo Alkhamisi katika mazungumzo yake ya simu na Rais Bashar al-Assad wa Syria na kuongeza kuwa, "Syria ni mshirika wa kistratejia na rafiki muaminifu wa taifa la Iran."

Ameipongeza serikali ya Damascus kwa kutangaza siku tatu za maombolezo ya kitaifa kufuatia kufa shahidi Rais Ebrahim Raisi wa Iran na maafisa wenzake, na vile vile hatua ya Syria ya kutuma ujumbe wa ngazi za juu ukiongozwa na Waziri Mkuu wa nchi hiyo ya Kiarabu kuja Tehran kushiriki mazishi ya viongozi hao wa Iran.

Mokhber ameongeza kuwa, risala ya rambirambi ya Rais Assad na ujumbe wa maafisa wa Syria hapa mjini Tehran kwa ajili ya kushiriki maombolezo umelifariji taifa la Iran wakati huu mgumu wa simanzi na majonzi. 

Katika mazungumzo hayo ya simu, Kaimu Raisi wa Iran amesisitiza kuwa Jamhuri ya Kiislamu itaendelea kuunga mkono kwa hali na mali kambi ya muqawama katika eneo hasa Syria.

Taifa la Iran limezama katika maombolezo wa viongozi wao waaminifu

Rais wa Syria, Bashari al-Assad kwa upande wake amelinyooshea taifa la Iran mkono wa pole kufuatia kufa shahidi Rais wa Iran Sayyid Ebrahim Raisi na Waziri wa Mambo ya Nje Hossein Amir-Abdollahian na ujumbe walioandamana nao.

Assad amesema: Kama alivyokuwa Shahidi Luteni Jenerali Qassem Soleimani, aliyekuwa Kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC), hayati Raisi alikuwa shakhsia mwenye ushawishi mkubwa katika eneo na duniani kote, na kumbukumbu yake itasalia kwenye fikra za taifa na serikali ya Syria.

Rais wa Syria amesema Sayyid Raisi alipambana na dhulma na ubeberu wa kimataifa na kuunga mkono mrengo wa muqawama, kama ambavyo aliyatetea mataifa madhulumu katika eneo na kote duniani, na vile vile kadhia ya Palestina.

Tags