Jun 17, 2024 05:59 UTC
  • Iran: Taarifa iliyotolewa na Troika ya Ulaya haina itibari

Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imekosoa vikali taarifa ya pamoja ya nchi tatu za Ufaransa, Ujerumani na Uingereza (Troika ya Ulaya) kuhusu mradi wa nyuklia wa Jamhuri ya Kiislamu wenye malengo ya amani na kusisitiza kuwa, taarifa hiyo imetolewa kwa kutegemea tuhuma bandia na zisizo na msingi.

Wizara hiyo imebainisha kuwa, taarifa ya nchi hizo tatu za Magharibi haina itibari, na kwamba "Mradi wa nyuklia wa Iran, kama inavayosisitiza mara kwa mara Jamhuri ya Kiislamu, una malengo ya amani; na silaha za nyuklia hazina nafasi katika doktrini ya kijeshi na kiulinzi ya Iran."

Wizara hiyo imesema Iran imeshikamana na inaheshimu ipasavyo ushirikiano wake na Wakala wa Kimataifa ya Nishati Atomiki IAEA chini ya Makubaliano ya Ulinzi, lakini inasikitisha kuona Uingereza, Ujerumani, na Ufaransa ambazo zina malengo na misimamo ya kiuadui dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu zinatumia vibaya ushirikiano huo wa kiufundi kuendeleza siasa zao za kibeberu na kupotosha ukweli wa mambo.

Imeeleza kuwa, taarifa hiyo ya nchi za Troika ya Ulaya inakosoa ushirikiano mzuri wa Iran na wakala wa IAEA huku ripoti karibu zote za wakala huo wa nyuklia zinaonesha kuwa Jamhuri ya Kiislamu imekuwa ikishirikiana vizuri nao. 

Troika ya Ulaya

Troika ya Ulaya juzi Jumamosi ilitoa taarifa ya pamoja na baada ya kukariri madai na tuhuma mbalimbali dhidi ya miradi ya nyuklia ya Iran yenye malengo ya amani, ilidai kuwa ina nia ya kupata ufumbuzi wa kidiplomasia ili kutatua shaka zilizopo kuhusu shughuli za nyuklia za Iran.  

Wizara ya Mambo ye Nje ya Iran imeongeza kuwa, kitendo chao hicho si kipya na wala hakishangazi kwani nchi hizo za Ulaya ni dhati yao kutoa tuhuma za uongo dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu.

Imesema ni kinaya kuona nchi tatu hizo za Ulaya zikidai kuwa Iran haitekelezi ahadi zake kwa mujibu wa mapatano ya nyuklia ya JCPOA katika hali ambayo, nchi hizo zinabeba dhima ya hali ya sasa ya mkwamo ya makubaliano hayo ya kimataifa. 

Tags