Zarif: Marekani ina utendaji dhaifu katika utekelezaji mapatano ya nyuklia na Iran
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i11518-zarif_marekani_ina_utendaji_dhaifu_katika_utekelezaji_mapatano_ya_nyuklia_na_iran
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Mohammad Javad Zarif amesema Marekani imekuwa na utendaji dhaifu katika kufungamana na mapatano ya nyuklia yaliyofikiwa mwezi Julai mwaka jana baina ya Iran na madola sita makubwa duniani ya kundi la 5+1.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Jul 19, 2016 04:22 UTC
  • Zarif: Marekani ina utendaji dhaifu katika utekelezaji mapatano ya nyuklia na Iran

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Mohammad Javad Zarif amesema Marekani imekuwa na utendaji dhaifu katika kufungamana na mapatano ya nyuklia yaliyofikiwa mwezi Julai mwaka jana baina ya Iran na madola sita makubwa duniani ya kundi la 5+1.

Katika mahojiano maalumu na Shirika la Utangazaji la Iran IRIB kwa munasaba wa kutimia mwaka wa kwanza wa kufikiwa mapatano ya nyuklia yajulikanayo kama Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezaji (JCPOA) ambayo yalifikiwa Julai 14 mwaka 2015 baina ya Iran na wanachama watano wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa yaani China, Russia, Uingereza, Ufaransa na Marekani pamoja na Ujerumani.

Zarif amesema JCPOA ni 'mafanikio muhimu sana kwa Jamhuri ya Kiislamu kwani yatalinda heshima ya taifa la Iran katika uga wa kimataifa, yatapelekea haki za Iran kutambuliwa sambamba na kubatilisha maazimio ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa dhidi ya Iran. Aidha amesema mapatano hayo pia yatazuia Iran kuwekewa vikwazo vipya. Mapatano hayo baina ya Iran na madola sita makubwa duniani yalianza kutekelezwa Januari 16.

Zarif amesema JCPOA ni mapatano ambayo yamethibitisha kuwa Iran haiwezi kulazimiwa kufanya chochote hata kupitia mashinikizo makubwa. Aidha amesema Iran itaendelea kutekeleza ahadi zake kwa mujibu wa JCPOA na kuongeza kuwa Tehran ina azma ya kuhakikisha upande wa pili unatekeleza ahadi zake. Aidha amesema baada ya kuanza kutekelezwa JCPOA, nchi nyingi za Ulaya zilibainisha hamu ya kufanya biashara na Iran. "Hata hivyo benki nyingi zinahofu kuadhibiwa na Marekani ( iwapo zitafanya biashara na Iran), hii ni hofu ya kisaikolojia kutokana na muelekeo wa kihafidhina wa taasisi za kifedha," amesema Zarif.

Pamoja na serikali ya Marekani kuidhinisha mapatano ya nyuklia ya JCPOA, lakini bunge la nchi hiyo, linalodhibitiwa na chama cha Republican, limepitisha miswada kadhaa ya sheria kwa lengo la kuvuruga mapatano hayo ambayo yanatizamwa kama turathi ya sera za kigeni za Rais Obama.