Aug 13, 2024 10:45 UTC
  • Iran yatilia mkazo wajibu wa kukomeshwa haraka mauaji ya Ukanda wa Ghaza

Kaimu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema kuwa, Tehran sambamba na kuendelea na jitihada zake za kuhakikisha utawala wa Kizayuni unakomesha mashambulizi na ukatili wake huko Ghaza, inashikilia pia haki yake ya dhati na ya kisheria ya kuchukua hatua yoyote itakayoona inafaa kujibu jinai za Israel.

Shirika la habari la IRNA limemnukuu Ali Baqeri Kani akisema hayo katika mazungumzo ya simu aliyofanya na Antonio Tajani, waziri wa mambo ya nje wa Italia na huku akiashiria jinai za kutisha za utawala wa Kizayuni dhidi ya wananchi wasio na hatia wa Ukanda wa Ghaza kwa miezi 10 sasa ameelezea kusikitisha na misimamo ya kihalifu ya viongozi wa utawala wa Kizayuni na waungaji mkono wao ya kueneza vitendo vyao vya kigaidi hadi nje ya ardhi za Palestina. 

Ameongeza kuwa, mashambulizi ya utawala wa Kizayuni kwenye ubalozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran mjini Damascus Syria, jinai ya Israel ya kushambulia kikatili jengo la ghorofa la makazi ya raia huko Beirut, Lebanon, kumuuua kigaidi mgeni rasmi mwenye hadhi ya kidiplomasia mjini Tehran Iran na kuendelea kukwamisha juhudi za kukomesha vita huko Ghaza yote hayo yanaifanya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuwa na nia thabiti zaidi ya kulinda haki zake mbele ya utawala dhalimu kama huo.  

Kwa upande wake, Waziri wa Mambo ya Nje wa Italia ameelezea wasiwasi wa nchi yake wa kuendelea mgogoro na ukosefu wa amani katika eneo hili na amezitaka pande husika kuvumiliana ili hali isiharibike zaidi. Vilevile ametilia mkazo haja ya kufanyika juhudi kubwa zaidi za kuhakikisha vita vinasimamishwa Ghaza na vile vile ameelezea hamu ya nchi yake ya kustawisha zaidi uhusiano wake na Iran.

Tags