Iran: Nchi za Kiislamu zinapaswa kuungana ikwa ajili kukabiliana na mauaji ya kimbari huko Gaza
(last modified Sat, 31 Aug 2024 08:00:09 GMT )
Aug 31, 2024 08:00 UTC
  • Iran: Nchi za Kiislamu zinapaswa kuungana ikwa ajili kukabiliana na mauaji ya kimbari huko Gaza

Mjumbe wa Kamisheni ya Usalama wa Taifa na Siasa za Kigeni ya Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu ya Iran (Bunge) ametoa wito wa kuwepo umoja miongoni mwa nchi za Kiislamu kwa ajili ya kukabiliana na jinai na mauaji ya kimbari ya utawala wa Kizayuni katika Ukanda wa Gaza.

Amir Hayat Moghadam, mjumbe wa Kamisheni ya Usalama wa Taifa na Siara za Kigeni ya Majlisi ya Kiislamu amegusia wimbi jipya la mashambulizi ya askari wa utawala wa Kizayuni wa Israel katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na kusini mwa Lebanon na kusema kuwa, nchi za Kiislamu zinapaswa kusimama imara katika kuunga mkono taifa madhulumu la Palestina dhidi ya utawala wa Israel.

Mbunge huyo wa Majlisi ya Kiislamu ya Iran ameeleza kuwa mashirika, taasisi na jumuiya za kimataifa hazitachukua hatua ya kuwatetea wananchi wasio na ulinzi wa Palestina huko Ukanda wa Gaza na kuongeza kuwa, haijawahi kutokea katika historia ambapo jinai kama hizo zinafanyika katika ardhi ndogo kama hiyo ambayo watu wake hawana silaha maalumu za kujilinda.

Mjumbe huyo wa Kamisheni ya Usalama wa Taifa na Siasa za Kigeni pia amesema Miinuko ya Golan ni eneo la kistratijia kaskazini mwa ardhi zinazokaliwa kwa mabavu, ambalo linapaswa kurejeshewa Syria, na ni muhimu kwa nchi za Kiislamu kuchukua hatua kuhusu suala hili.

Tangu Oktoba 7 mwaka jana na kwa uungaji mkono kamili wa nchi za Magharibi, utawala wa Kizayuni wa Israel umefanya mauaji makubwa ya umati katika Ukanda wa Gaza na Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan dhidi ya wananchi wasio na ulinzi na madhulumu wa Palestina, ambapo kimya cha jumuiya na taasisi za kimataifa zinazodai kutetea haki za binadamu mbele ya jinai za utawala ghasibu wa Israel kimepelekea kuendelea kuchinjwa kikatili wanawake na watoto wa Kipalestina na utawala huo haramu.