Sep 07, 2024 02:30 UTC
  • Maghala ya nyuklia ya Israel tishio kubwa kwa amani na usalama wa dunia

Balozi na mwakilishi wa kudumu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika Umoja wa Mataifa amesema kuwa, silaha za nyuklia za utawala wa Kizayuni wa Israel ni tishio kubwa kwa amani na usalama wa kikanda na wa ulimwengu mzima.

Amir Saeed Iravani amesema hayo katika kikao cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kilichofanyika kwa mnasaba wa kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Kupambana na Majaribio ya Nyuklia na kubainisha kuwa, kuadhimisha siku hiyo ni fursa kwa Jamii ya Kimataifa ya kuulazimisha utawala wa Israel ujiunge bila ya masharti yoyote na Mkataba wa Kuzuia Uenezaji Silaha za Nyuklia (NPT) na kuviweka vituo vyake vyote vya nyuklia chini ya usimamizi kamili wa Wakala wa Kimataifa la Nishati ya Atomiki (IAEA).

Iravani ameongeza kuwa, hali ya sasa inatia wasiwasi, kwa sababu utawala wa Israel unazitishia nchi za eneo kwa maangamizi ya kinyuklia; na maghala ya silaha zake za nyuklia ni tishio kubwa kwa amani na usalama wa kieneo na kimataifa.

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, ikiwa moja ya nchi zilizotia saini mkataba wa kukabiliana na majaribio ya nyuklia CTBT, inauchukulia mkataba huo kuwa hatua moja mbele kuelekea katika utokomezaji wa silaha za nyuklia; na kuhusiana na suala hilo inaitakidi kwamba, mkataba wa CTBT hauwezi kuchukua nafasi ya utokomezaji kamili wa silaha za nyuklia, kwa hivyo, utokomezaji wa silaha za nyuklia inapasa uendelee kuwa kipaumbele kikuu cha Jamii ya Kimataifa; na aina zote za majaribio ya nyuklia inapasa zipigwe marufuku kikamilifu.

Kiwanda cha nyuuklia cha Israel cha Dimona

 

Kulingana na ripoti za kimataifa, takriban majaribio 2,000 ya nyuklia yamefanywa tangu 1945, ambapo Marekani pekee imefanya majaribio 1,054 na inaendelea kupanua mipango yake ya nyuklia. Tangu mwaka 1950, kwa usaidizi wa Ufaransa na Marekani, utawala wa Kizayuni umekuwa tishio kwa eneo na walimwengu kwa kuendeleza miradi ya nyuklia, ukiwemo ujenzi wa kituo cha nyuklia cha "Dimona" na uundaji wa makumi ya vichwa vya nyuklia.

Shughuli hizo zinaendelea kupanuliwa huku utawala ghasibu wa Israel ukiwa umekataa katakata kuruhusu ukaguzi wa aina yoyote kwa vituo vyake haramu vya nyuklia na haujatia saini Mkataba wa Kuzuia Uundaji na Uenezaji wa Silaha za Nyuklia (NPT). Katika mazingira hayo, nchi za Magharibi zikiongozwa na Marekani zimetekeleza vikwazo vya kikatili dhidi ya Iran katika miaka ya hivi karibuni kwa kisingizio cha kuendeleza taifa hili miradi yake ya nyuklia ambayo kimsingi inafanyika kwa malengo ya amani.

Hadi leo utawala dhalimu wa Israel umekataa kujiunga na Mkataba wa Kuzuia Uundaji na Uenezaji wa Silaha za Nyuklia (NPT).

 

Madai ya uzushi ya Marekani, Ulaya na Israel kuhusu shughuli za amani za nyuklia za Iran yanatolewa katika katika hali ambayo, ufuatiliaji na uangalizi wa shughuli za nyuklia za Iran kinyume na Israel unafanyika mara kwa mara na Iran imekuwa ikitoa ushirikiano kwa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA)  ambao wakati mwingine ni wa hiari na ulioko juu zaidi ya kiwango cha kawaida. Rafael Grossi, Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA), amesisitiza mara kwa mara kuhusu ushirikiano mzuri wa Iran kwa wakala huo.

Fauka ya hayo, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa kuzingatia itikadi zake za kidini na kimaadili, imetangaza kwa walimwengu kuwa ni haramu kutengeneza na kutumia silaha za nyuklia na imelisajili suala hilo kuwa hati rasmi katika Umoja wa Mataifa.

Pamoja na hayo yote, kuendelea kelele za kipropaganda na anga za uongo za nchi za Magharibi dhidi ya shughuli za amani za nyuklia za Iran, kunaonesha kuwa, nchi hizo zinajaribu kugeuza fikra za umma kutoka katika maghala yao ya silaha za nyuklia na utawala wa Kizayuni kwa kuchafua na kurudiarudia madai yasiyo na msingi wala ukweli dhidi ya Tehran na hivyo kuitambulisha Iran kama nchi mkosa  katika masuala ya nyuklia.

Rafael Grossi, Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA)

 

Licha ya njama hizo, lakini suala la silaha za nyuklia za utawala wa Kizayuni limekuwa miongoni mwa kero kubwa za nchi za eneo la Magharibi mwa Asia kwa miongo kadhaa, na nchi nyingi za eneo hili zimekuwa zikitaka kuangamizwa silaha hizo.

Israel, ambayo tangu mwanzo imekuwa moja ya tawala zilizojilimbikizia zaidi silaha za nyuklia na wakati huo huo za siri zaidi ulimwenguni, haijakubali kujiunga na mkataba wa Kuzuia Uundaji na Uenezaji wa Silaha za Nyuklia (NPT). Hatua hiyo ya Israel imeufanya utawala huo daima uandamwe kwa tuhuma za nchi za kikanda na pia katika ngazi ya kimataifa. Kwa mujibu wa makadirio mbalimbali, utawala wa Kizayuni unamilikki vichwa 80 hadi 200 vya silaha za nyuklia. Hadi sasa Israel imekataa na kupuuza miito yote ya kuitaka ijiunge na mkataba wa NPT na wakati huo huo kuendelea kupanua mipango na miradi yake ya nyuklia.

Kwa hakika Marekani ikiwa ni mshirika wa kistratijia wa Israel si tu kwamba imekuwa miongoni mwa wasambazaji wakuu wa nyenzo na zana za nyuklia kwa utawala wa Kizayuni, bali daima imekuwa ikizuia mashinikizo yoyote dhidi ya utawala huo yanayoitaka ijiunge na mkataba wa NPT.

Tags