Sep 18, 2024 06:13 UTC
  • Rais Pezeshkian wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran: Hatupendi vita, tunatetea haki zetu

Rais Masoud Pezeshkian wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema, Iran haijawahi kuwa, na wala haitakuwa mwanzishaji vita vyovyote vile na akabainisha kwamba: "wiki ijayo tutatetea haki za wananchi wa Iran katika Umoja wa Mataifa".

Rais Pezeshkian ameyasema hayo baada ya kuhudhuria bungeni hapo jana na akaongeza kuwa, "katika kipindi cha miaka 200 iliyopita, hutaona hata mara moja katika historia, kwamba Iran imeivamia nchi, lakini wao wamejenga taswira isiyo ya kiinsafu kuhusiana na sisi".
 
Akizungumzia hatua ya kuizushia Iran matatizo mbalimbali na vikwazo, Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema: "wameanzisha utawala wa Kizayuni katika eneo na kuuzatiti kikamilifu kwa silaha, kisha wanatuambia sisi hamtakiwi kuwa na silaha yoyote, ili Wazayuni waweze kutupiga kwa mabomu wakati wowote watakapotaka."

Pezeshkian ameongezea kwa kusema: "ikiwa wanachotaka ni kuonyesha ubabe, sisi hatutaupigia magoti ubabe na utumiaji mabavu."

 
Rais Masoud Pezeshkian wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, wiki ijayo ataelekea New York kuhudhuria na kuhutubia mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.
 
Kuhutubia kikao kidogo cha Baraza Kuu kitakachofanyika kwa anuani ya "Viongozi kwa ajili ya Mustakabali", kukutana na Wairani wanaoishi Marekani, kufanya mazungumzo na viongozi wa kidini, kukutana na wakuu wa vyombo vya habari na wa taasisi za wanafikra na mazungumzo mengine ya pande mbili na baadhi ya wakuu wa nchi za Ulaya, Asia na  za Ulimwengu wa Kiislamu, ni miongoni mwa ratiba zingine anazotazamiwa kuwa nazo Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika safari yake ya New York.../

 

Tags