Ayatullah Khatami: Bahrain inawakandamiza wananchi kwa usimamizi wa Marekani na Uingereza
Khatibu wa Swala ya Ijumaa iliyoswaliwa leo hapa mjini Tehran amesema kuwa, watawala wa Aal Khalifa wamekuwa wakiamialiana vibaya na raia wa Bahrain kwa usimamizi wa Marekani na Uingereza.
Ayatullah Sayyid Ahmad Khatami amesema hayo leo mbele ya hadhara kubwa ya waumini waliohudhuria ibada ya Swala ya Ijumaa mjini Tehran na ambapo sambamba na kuashiria matukio ya hivi karibuni nchini Bahrain na kupokonywa uraia Sheikh Issa Qassim mwanazuoni mashuhuri wa nchi hiyo amebainisha kwamba, watawala madikteta na madhalimu wa Bahrain wamekuwa wakitenda kila aina ya jinai dhidi ya raia wa nchi hiyo.
Khatibu wa Swala ya Ijumaa mjini Tehran amesema kuwa, kwa mujibu wa vipengee vingi vya haki za binadamu, hakuna utawala ambao una haki ya kumpokonya uraia raia yeyote lakini inasikitisha kuona kwamba, watawala wa Manama wamempokonya raia mwanazuoni huyo.
Ayatullah Ahmad Khatami ameitaja ripoti ya Ban Ki-moon Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusiana na utekelezwaji wa makubaliano ya nyuklia kati ya Iran na madola sita makubwa duniani kwamba, haina insafu wala uadilifu.
Amesema, Katibu Mkuu ambaye anaandaa ripoti kwa mashinikizo ya Wazayuni na anapokea dola za Saudi Arabia ili aliondoe jina la nchi hiyo katika orodha ya wakiukaji wa haki za binadamu na wauaji wa watoto wasio na hatia wa Yemen hatarajiwi kitu kingine ghairi ya hiki.