Spika wa Bunge la Iran awasili Ethiopia kwa ziara rasmi
Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge la Iran) amewasili Addis Ababa, mji mkuu wa Ethiopia akiongoza ujumbe wa ngazi za juu Bunge kwa mwaliko wa Spika wa Baraza la Wawakilishi la Ethiopia.
Mwandishi wa Radio Tehran ameripoti kuwa, Mohammad Bagher Ghalibaf, Spika wa Bunge la Iran amewasili Addis Ababa mji mkuu wa Ethiopia na kupokewa na viongozi mbalimbali akiwemo pia balozi na wanadiplomasia wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran nchini humo.
Ziara hiyo imefanyika kwa mwaliko wa Spika wa Baraza la Wawakilishi la Ethiopia, Tagse Shafaw, ikiwa ni sehemu ya harakati za kidiplomasia za mabunge ya nchi hizi mbili kwa ajili ya kuimarisha nafasi ya bunge katika sera za kigeni, kukuza uchumi na utamaduni na kuimarisha mahusiano ya kisiasa kati ya nchi hizo mbili.
Kutembelea Makumbusho ya Vita ya Adwa na kukutana na wafanyabiashara wa Iran wanaoishi Ethiopia itakuwa miongoni mwa ratiba za siku ya kwanza ya ziara ya Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge la Iran) mjini Addis Ababa.
Ethiopia ina nafasi maalumu katika siasa na uchumi wa Afrika kutokana na kuwa ni moja ya nchi kongwe huru barani humo na mwenyeji wa mashirika muhimu ya kimataifa. Ina idadi kubwa ya watu, ni mwanachama wa mashirika ya kimataifa kama vile kundi la BRICS, ina makao makuu ya Umoja wa Afrika AU na inachukuliwa kuwa moja ya nchi muhimu na zenye ushawishi mkubwa barani Afrika.