Rais Pezeshkian: Iran haitasalimu amri kwa vitisho na vikwazo
(last modified Fri, 24 Jan 2025 06:59:56 GMT )
Jan 24, 2025 06:59 UTC
  • Rais Pezeshkian: Iran haitasalimu amri kwa vitisho na vikwazo

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, taifa hili halitasalimu amri kwa vitisho na vikwazo vya maadui.

Rais Masoud Pezeshkian amesema hayo katika hadhara ya wasomi na wenye vipawa katika mkoa wa Khuzestan, kusini-magharibi mwa Iran ambapo ameashiria vitisho vya maadui dhidi ya wananchi wa Iran na kusisitiza kuwa taifa la Iran halitasalimu amri mbele ya vitisho na vikwazo.

Kadhalika amesema, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haina ugomvi au vita na nchi yoyote ile bali inataka kuweko hali ya kuishi kwa amani na utulivu.

Daktari Pezeshkian amefafanua kuwa, Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema katika sera kuu za mfumo unaotawala hapa nchini kwamba,  inapasa kuanzisha uhusiano na nchi zote za dunia kwa kuzingatia misingi mitatu ya heshima, manufaa na hekima isipokuwa utawala dhalimu wa Israel unaokalia kwa mabavu Palestina ambao hauthamini utu na ubinadamu.

Rais wa Iran ameongeza kuwa, katika hali ambayo utawala wa Kizayuni wa Israel uliua shahidi maelfu ya watu wasio na hatia katika Ukanda wa Gaza kwa uungaji mkono wa mataifa ya kibeberu, waungaji mkono wa utawala huo ghasibu wanajitokeza na kuzungumzia haki za binadamu, huku waungaji mkono wa utawala huo wakiunga mkono mauaji ya kimbari ya utawala ghasibu wa Israel.