Imam Khamenei apongeza ujasiri wa wananchi wa Lebanon
Akaunti rasmi ya mtandao wa kijamii wa X ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Sayyid Ali Khamenei imetuma ujumbe kufuatia kitendo cha kijasiri cha wananchi wa Lebanon kusini mwa nchi hiyo ya Kiarabu.
Ayatullah Sayyid Ali Khamenei amesema katika ujumbe huo uliotumwa leo Jumatatu kuwa: "Mahesabu yote ya kisiasa na ya kimaslahi leo yamethibiti kuwa hayana nguvu mbele ya wakazi waaminifu wa kusini mwa #Lebanon ambao hawakutikiswa hata kidogo na jeshi la utawala wa Kizayuni."
Vikosi vya Israel jana viliwafyatulia risasi na kuwaua Walebanon kadhaa waliokuwa wamekimbia makazi yao kusini mwa Lebanon na waliokuwa wakirejea katika miji yao, huku muhula wa mwisho wa kuondoka askari hao makatili ukimalizika.
Ujumbe huo wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu umemalizia kwa kusema: Imani thabiti ya Walebanon katika ahadi ya Mungu iliwawezesha kuweka maisha yao kwenye mstari (hatarini).
Wakati huo huo, Ofisi ya Waziri Mkuu wa muda wa Lebanon, Najib Mikati, imetangaza kurefusha makubaliano ya kusitisha mapigano ya Novemba 2023 katika nchi hiyo ya Kiarabu.
Uamuzi wa kuongeza muda huo ulifanywa baada ya kushauriana na Spika wa Bunge la Lebanon Nabih Berri na Rais Joseph Aoun na kuwasiliana na upande wa Marekani.

Kamati ya utendaji itafuatilia utekelezaji wa makubaliano ya kusitisha mapigano kwa kuzingatia Azimio Nambari 1701 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. Kama Lebanon ilivyoomba, Marekani itaanzisha mazungumzo ya kuachiliwa kwa wale waliokamatwa na utawala wa Israel tangu Oktoba mwaka 2023.
Kwa mujibu wa makubaliano ya kusitisha mapigano, muhula wa siku 60 wa kuondoka kabisa vikosi vya utawala wa Kizayui wa Israeli kutoka Lebanon ulimalizika jana Jumapili, Januari 26.