Kiongozi Muadhamu: Maandamano dhidi ya Israel yanaashiria kuungwa mkono zaidi Palestina duniani
(last modified Sat, 22 Feb 2025 12:06:32 GMT )
Feb 22, 2025 12:06 UTC
  • Kiongozi Muadhamu: Maandamano dhidi ya Israel yanaashiria kuungwa mkono zaidi Palestina duniani

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Sayyid Ali Khamenei amesema maandamano na mikusanyiko dhidi ya Israel barani Ulaya na Marekani inaashiria kuongezeka mshikamano wa kimataifa na taifa la Palestina.

Akizungumza katika kikao na maafisa wa Wizara ya Usalama ya Iran siku ya Jumatano, Ayatullah Khamenei alisema mikusanyiko ya hivi karibuni dhidi ya Israel katika nchi za Ulaya na Marekani inadhihirisha kwamba, maoni ya umma duniani kote yanaelekea zaidi katika kuwaunga mkono watu wa Palestina; na hilo ni dhihirisho la irada ya Allah.

Kiongozi Muadhamu amepongeza pia maandamano matukufu yaliyofanyika kote Iran tarehe 10 Februari (Bahman 22), kuadhimisha mwaka wa 46 wa Ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu.

Ayatullah Ali Khamenei ameeleza bayana kuwa, hivi sasa fikra za walimwengu zinaelekea zaidi katika kuiunga mkono, kuihami na kuitetea Palestina. 

Imam Khamenei amesisitiza umuhimu wa kupanga mikakati ya kutatua masuala ya ndani na kusema kuwa, jukumu la Wizara ya Usalama ni kushirikiana na serikali kuendesha nchi.

Kiongozi Muadhamu katika mkutano na maafisa wa Wizara ya Usalama ya Iran

Ayatullah Khamenei ameeleza bayana kuwa, kushughulikia masuala katika sekta za kiuchumi, kisiasa, kiutamaduni na kijamii kunategemea imani kwa Mwenyezi Mungu, kushikamana na misingi ya Mapinduzi ya Kiislamu, kufuatilia kwa bidii mipango na sheria zilizopo nchini, na kufidia mambo na mipango iliyoakhirishwa au kucheleweshwa.

Kadhalika Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika mkutano huo na maafisa wa Wizara ya Usalama wa Iran alisisitiza umuhimu wa kubuni mipango madhubuti ya kushughulikia masuala ya kitaifa.