Trump adai yuko tayari kukutana na Kiongozi Muadhamu wa Iran
(last modified Sat, 26 Apr 2025 02:39:05 GMT )
Apr 26, 2025 02:39 UTC
  • Trump adai yuko tayari kukutana na Kiongozi Muadhamu wa Iran

Rais wa Marekani Donald Trump amesema yuko tayari kukutana na Rais wa Iran, Masoud Pezeshkian au Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, amesema hayo katika mahojiano na TIME.

Kwengineko kwenye mahojiano hayo na gazeti la TIME, Trump amesema "Nadhani tutafikia makubaliano na Iran." Shirika la habari la Mehr limeandika habari hiyo na kumnukuu Trump akieleza kuwa, Waziri Mkuu wa utawala wa Israel, Benjamin Netanyahu hawezi kuiburuza Marekani katika vita na Iran.

Trump ameyasema hayo kabla ya kuanza duru ya tatu ya mazungumzo ya nyuklia yasiyo ya moja kwa moja kati ya Tehran na Washington, iliyopangwa kufanyika nchini Oman leo Jumamosi.

Mapema jana Ijumaa, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, Esmaeil Baghaei alisema kuwa, Tehran na Washington zimefikia maelewano ya kufanya vikao vya kiufundi na vya kitaalamu sambamba na kuwepo wapatanishi wakuu kutoka Iran na Marekani.

Kwa mujibu wa mipango iliyofanywa na Oman, mwenyeji na mpatanishi wa mazungumzo hayo, na kuafikiwa na Tehran na Washington, mikutano ya kiufundi na mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja kati ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran na Mjumbe Maalum wa Rais wa Marekani yamepangwa kufanyika Jumamosi, Baghaei amesisitiza.

Msemaji huyo wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Iran amesisitiza kuwa, maendeleo katika mazungumzo hayo ya Oman yanategemea irada ya kisiasa na nia njema, uhalisia na umakini utakaoonyeshwa na upande wa pili.

Amesisitiza kuwa, ujumbe wa Iran utafuatilia kila hatua ya mazungumzo hayo kwa kuzingatia tajriba na mwenendo wa Marekani, na utafanya juu chini kulinda haki na maslahi halali ya wananchi wa Iran.