Baqaei atangaza mabadiliko katika ratiba ya mazungumzo ya Iran na Marekani
Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ametangaza kubadilishwa tarehe ya duru ijayo ya mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja ya Iran na Marekani ambayo yalipangwa kufanyika Jumamosi ya tarehe 4 Mei huko Roma, mji mkuu wa Italia.
Akiashiria tangazo la Waziri wa Mambo ya Nje wa Oman, Ismail Baqaei, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema kwamba kuahirishwa kwa mazungumzo hayo kunatokana na pendekezo la Waziri wa Mambo ya Nje wa Oman na kwamba taarifa kuhusu tarehe inayofuata itatolewa baadaye.
Baqaei, amesisitiza tena irada na azma ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ya kutumia diplomasia ili kudhamini maslahi halali na ya kisheria ya wananchi wa Iran na kukomesha vikwazo na mashinikizo ya kiuchumi ambayo yanalenga haki za binadamu na ustawi wa kila Muirani.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ameeleza kuwa: Tangu mwanzo wa mazungumzo hayo, ujumbe wa Tehran umeainisha misingi maalumu kwa kuzingatia misimamo ya Iran kwa mujibu wa sheria za kimataifa katika uga wa matumizi ya amani ya nishati ya nyuklia na kuhitimisha vikwazo vilivyo kinyume cha sheria, na umeonyesha azma yake kubwa katika mazungumzo yenye mwelekeo wa matokeo ili kufikia maelewano ya haki, ya kuridhisha na endelevu, na utaendelea kuwa imara katika njia hii kwa nguvu zote.
Duru ya tatu ya mazungumzo yasiyo ya ana kwa ana kati ya wawakilishi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Marekani, ilifanyika wiki iliyopita Muscat, mji mkuu wa Oman kwa uratibu wa serikali ya nchi hiyo.