Iran yaambia Marekani: Urutubishaji madini ya urani 'hauwezi kujadiliwa'
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema kwamba taifa la Iran halitikisiki mbele ya mbinu za mashinikizo za Marekani, na kutupilia mbali madai ya Washington yanayotaka Jamhuri ya Kiislamu iachane na haki yake halali ya kutumia nishati ya nyuklia kwa malengo ya amani.
Esmaeil Baghaei katika mahojiano na CNN, kama ilivyoripotiwa kwenye tovuti ya kituo hicho amesema, "Wairani hawatalegezwa kwa mashinikizo yoyote."
"Mnapozungumza kwa lugha ya mashinikizo, Wairani husimama kwa sauti moja, na hakika tutalinda usalama wetu wa kitaifa," ameongeza.
Afisa huyo alikuwa akizungumzia msimamo wa mara kwa mara wa maafisa tofauti wa Marekani wanaotaka Iran iachane kabisa na shughuli zake za kurutubisha madini ya urani ambayo ni muhimu katika sekta ya nyuklia.
Amebaini kuwa: "Kama lengo la Marekani ni kuwanyima Wairani haki yao ya kutumia nishati ya nyuklia kwa matumizi ya amani, basi hilo litakuwa tatizo kubwa kiasi kwamba linaweza kuhatarisha mchakato mzima."
Baghaei alikuwa akiashiria mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja yanayoendelea kwa upatanishi wa Oman kati ya pande hizo mbili tangu Aprili 12.
Amebaini kuwa: "Ukweli kwamba hadi sasa tumeendelea na mazungumzo unaonyesha kuwa kuna kiwango fulani cha maelewano kwamba Iran haiwezi, kwa hali yoyote ile, kuachana na haki yake ya kutumia nishati ya nyuklia kwa njia ya amani."
Marekani, pamoja na mshirika wake mkuu wa eneo hili – utawala wa Kizayuni wa Israel – wamekuwa wakisisitiza mara kwa mara kuwa Iran isitishe kabisa shughuli zake za nyuklia za amani.
Licha ya mashinikizo hayo, Tehran imesimama imara kutetea haki yake ya kiuhuru ya kuendeleza programu ya nyuklia kwa matumizi ya kiraia.
Hivi karibuni, Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi ya Kiislamu, alisema kuwa "ni makosa makubwa" kwa Marekani kushinikiza kusitishwa mpango wa Iran wa kurutubisha urani kwa ajili ya matumizi ya amani, akisisitiza kwamba Jamhuri ya Kiislamu haina haja ya ruhusa kutoka kwa taifa lolote la kigeni ili kuendeleza shughuli zake hizo.
Baghaei amesisitiza kuwa bado kuna uwezekano wa pande mbili kufikia muafaka.