'Umoja kati ya dini za Ibrahim ndilo jibu pekee kwa dhulma duniani'
Umoja miongoni mwa dini za Nabii Ibrahim AS ndilo jibu pekee la ufanisi mkabala wa kuongezeka kwa dhulma na ukosefu wa haki na uadilifu duniani.
Hayo yalisemwa jana Jumatano na Mohammad Hassan Akhtari, Mkuu wa Baraza Kuu la Jumuiya ya Kimataifa ya Ahlul-Bayt, katika mkutano uliofanyika hapaTehran. Mkutano huo uliojumuisha wanazuoni wa Kishia, Sunni na Wayahudi ulichunguza hatua za kivitendo za kupinga uchokozi wa Marekani na Israel dhidi ya Iran.
Akhtari amesifu na kupongeza taarifa za hivi karibuni za kuunga mkono Iran kutoka kwa shakhsia mbali mbali wa kidini kama vile Ayatullah Ali Sistani wa Iraq na Imam Mkuu wa Chuo Kikuu cha Kiislamu cha Al-Azhar cha Misri, Ahmed el-Tayyeb; lakini amesisitiza kwamba matamko pekee hayatoshi.
Amewataka viongozi wa kidini kubadilisha miito ya mshikamano kuwa hatua madhubuti dhidi ya ukandamizaji na dhulma duniani. Vile vile amezitaka mamlaka za Kikristo, akirejelea matumizi mabaya ya matamshi ya kidini na Rais wa Marekani Donald Trump, kuueleza umma kuwa viongozi wa kisiasa kama Trump hawawakilishi maadili halisi ya Ukristo.
Hali kadhalika Mkuu wa Baraza Kuu la Jumuiya ya Kimataifa ya Ahlul-Bayt amewataka viongozi wa Kikristo kumpinga Trump na matumizi yake ya hotuba za kidini kufikia malengo ya kisiasa.
Kabla ya hapo, kundi la wanazuoni na wasomi 100 wa Kiislamu kutoka sehemu mbalimbali duniani walitoa tamko rasmi wakimtangaza Rais wa Marekani Donald Trump na Waziri Mkuu wa utawala haramu wa Israel Benjamin Netanyahu kuwa maadui wanaopigana na Mwenyezi Mungu, na ni waharibifu katika ardhi.