Iran, Troika ya Ulaya kuendelea na mazungumzo ya nyuklia wiki ijayo?
Iran na Troika ya Ulaya - Ufaransa, Ujerumani, na Uingereza - zimeripotiwa kukubaliana msingi wa kuanza tena mazungumzo ya nyuklia wiki ijayo.
Chanzo cha habari kililiambia shirika la habari la Tasnim jana Jumapili kwamba, pande hizo mbili zimekubali kuanza tena mazungumzo, lakini wakati na mahali pa mazungumzo hayo bado hayajaamuliwa.
Duru hizo za habari zimeeleza bayana kuwa, "Kanuni ya mazungumzo imekubaliwa, lakini mashauriano yanaendelea kuhusu muda na mahali pa kufanyika mazungumzo hayo."
Nchi ambapo mazungumzo hayo yanaweza kufanyikia bado haijaafikiwa," kimesema chanzo hicho. Kwa mujibu wa chanzo hicho, mazungumzo hayo yatafanyika katika ngazi ya mawaziri wa mambo ya nje.
Katika mazungumzo na wenzake wa Ujerumani, Ufaransa, na Uingereza na mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya Kaja Kallas siku ya Alkhamisi, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araghchi alisema Umoja wa Ulaya na Troika ya Ulaya zinapaswa kuachana na "sera zao chovu" za vitisho na mashinikizo ikiwa zinataka kuwa na jukumu katika duru yoyote mpya ya mazungumzo ya nyuklia kati ya Iran na Marekani.
Akiashiria vitisho vya mara kwa mara vya Ulaya kuhusu uanzishaji wa utaratibu ambao utaiwekea tena Jamhuri ya Kiislamu vikwazo vikali, Araghchi alisema, "Ikiwa EU/E3 zinataka kuwa na jukumu, zinapaswa kuchukua hatua kwa uwajibikaji, na kuweka kando sera zao chakavu za vitisho na mashinikizo, ikiwa ni pamoja na vitisho vya kuhuisha mchakato wa kuirejeshea Iran vikwazo vya Umoja wa Mataifa, mchakato ambao hawana kabisa msingi wa kimaadili na kisheria kuufufua.
"Mazungumzo yoyote mapya yanawezekana tu wakati upande mwingine uko tayari kwa makubaliano ya nyuklia ya haki, yenye uwiano na yenye manufaa kwa pande zote," aliongeza Araghchi.