Velayati: Shambulizi la Qatar laonesha kuwa Israel ‘haina mipaka’ katika uhalifu wake
Mshauri mwandamizi wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Seyyed Ali Khamenei, amesema kuwa dunia haiwezi kuendelea kufumbia macho ukatili wa Israel kufuatia mashambulizi yake ya kikatili dhidi ya Qatar, akieleza kuwa utawala huo haramu “hautambui mipaka” katika uhalifu wake.
Ali Akbar Velayati, mshauri wa Kiongozi Muadhamu katika masuala ya kimataifa, alitoa kauli hiyo kupitia chapisho la lugha ya Kifarsi kwenye mtandao wa kijamii wa X, baada ya shambulizi la kigaidi la Israel tarehe 9 Septemba katika mji mkuu wa Qatar, Doha, ambalo liliwaua maafisa kadhaa wa Hamas pamoja na raia wa Qatar.
Velayati ambaye aliwahi kuwa waziri wa mambo ya nje wa Iran ameendelea kuandika kuwa: “Uvunjaji wa sheria za kimataifa na kuingilia uhuru wa mataifa umekuwa jambo la kawaida kwa Wazayuni, na dunia lazima ivunje ukimya kuhusu jinai hizo."
Amebaini kuwa: “Kwa mara nyingine tena, kila mtu ameona kuwa utawala wa kikatili wa Kizayuni hautambui mipaka katika uhalifu wake." Aidha ameandika: “Shambulizi dhidi ya ardhi ya Qatar na ndugu wa Kipalestina waliokuwa kwenye mkutano ni jambo la kusikitisha na la kulaumiwa.”
Wakati huo huo, balozi na mwakilishi wa kudumu wa Iran katika Umoja wa Mataifa amesema kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inaunga mkono kwa dhati haki ya Qatar kujilinda dhidi ya uchokozi wa hivi karibuni wa Israel ulioilenga uongozi wa kisiasa wa Harakati ya Kiislamu ya Kupigania Ukombozi wa Palestina, Hamas, ndani ya ardhi yake.
Amir Saeed Iravani alitoa kauli hiyo siku ya Alhamisi katika taarifa iliyotayarishwa kwa ajili ya kikao cha dharura cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa (UNSC) kujadili mashambulizi ya Israel ya tarehe 9 Septemba dhidi ya mji mkuu wa Qatar, Doha, ambayo yaliwaua maafisa kadhaa wa Hamas pamoja na raia wa Qatar.
Amesema: “Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inalaani vikali na bila kusita mashambulizi ya kigaidi na ya kivita yaliyofanywa na utawala wa Kizayuni dhidi ya serikali ya Qatar, ambayo yamesababisha kuuawa na kujeruhiwa kwa raia wa Kipalestina na wa Qatar. Iran inatangaza mshikamano na uungaji mkono wake kwa serikali ya Qatar."
Aidha amesisitiza kuwa mashambulizi ya Israel dhidi ya Qatar na mataifa mengine ya eneo hilo ni ukiukaji wa wazi wa misingi ya Mkataba wa Umoja wa Mataifa na sheria za kimataifa.
Ameongeza kuwa: “Ni jambo la kusikitisha kwamba Baraza la Usalama, kwa kupuuza majukumu yake, limefanya uhalifu wa utawala wa Kizayuni huko Gaza na mashambulizi yake ya kijinai huko Yemen, Syria, Lebanon, Iran, na sasa Qatar kuwa jambo la kawaida.”
Balozi wa Iran na mwakilishi wa kudumu katika Umoja wa Mataifa amesisitiza kuwa kushindwa kwa Baraza la Usalama kuchukua hatua katika wakati huu nyeti ni uzembe mkubwa wa majukumu yake na ni usaliti wa misingi ambayo Umoja wa Mataifa ulianzishwa juu yake.