Iran yazionya Uingereza, Ufaransa, na Ujerumani kuhusu vikwazo
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araghchi, ametoa onyo kali kwa Uingereza, Ufaransa, na Ujerumani kwamba iwapo zitaendeleza juhudi zao za kuanzisha tena vikwazo vya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa dhidi ya Iran, basi zitakumbwa na madhara yasiyoweza kurekebishwa.
Mwanadiplomasia huyo wa ngazi za juu wa Iran alitoa kauli hiyo kupitia ujumbe aliouandika kwenye X (zamani Twitter) siku ya Jumamosi, akizilenga nchi hizo tatu ambazo ni sehemu ya makubaliano ya nyuklia ya mwaka 2015 na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, na sasa zinajaribu kutumia utaratibu unaojulikana kama "snapback" ili kurejesha vikwazo vilivyokuwa vimeondolewa.
Iran, pamoja na washirika wake wa kimkakati, yaani Russia na China, ambazo pia zilitia saini mapatano hayo ya nyuklia yajulikanayo kama JCPOA, zimekuwa zikisisitiza mara kwa mara kwamba kushindwa kwa mataifa ya Ulaya kutekeleza wajibu wao chini ya makubaliano hayo, ikiwemo kuzuia kurejeshwa kwa vikwazo, kunafuta kila msingi wa kutumia utaratibu huo wa "snapback."
Araghchi amesisitiza kuwa troika hiyo ya Ulaya (Uingereza, Ufaransa, na Ujerumani) haina msingi wa kisheria, kisiasa, wala kimaadili wa kurejesha vikwazo hivyo, akionya kuwa hatua hiyo itazua madhara makubwa yasiyoweza kurekebishwa.
Iran imetahadharisha kuwa iwapo troika hiyo itafaulu kutumia utaratibu huo wa kurejesha vikwazo, basi nchi hii itachukua hatua kali za kulipiza kisasi.
Hatua ambazo Iran inatarajiwa kuchukua zinajumuisha kusitisha makubaliano ya hivi karibuni kati ya Iran na Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki (IAEA), yaliyolenga kuimarisha ushirikiano wa kiufundi na wa kisera kati ya pande hizo mbili.
Kwa mujibu wa maafisa wa Iran, chaguo jingine lililo wazi ni kujitoa kabisa katika Mkataba wa Kutokuwa na Silaha za Nyuklia (NPT).
Aidha, siku hiyo ya Jumamosi, Waziri wa Mambo ya Nje alitoa maelezo kuhusu makubaliano hayo na IAEA katika mkutano wa dharura na wanachama wa Kamati ya Usalama wa Taifa na Sera za Nje ya Majlis (Bunge la Iran).
Akizungumza na waandishi wa habari pembezoni mwa mkutano huo, Ebrahim Azizi, mwenyekiti wa kamati hiyo, alieleza uwezekano wa Iran kujiondoa katika NPT iwapo mataifa ya Ulaya yatashindwa kutimiza ahadi zao.