Balozi wa Iran UN akosoa siasa za upande mmoja za madola makubwa
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i1333-balozi_wa_iran_un_akosoa_siasa_za_upande_mmoja_za_madola_makubwa
Balozi na mwakilishi wa kudumu wa Iran katika Umoja wa Mataifa amesema madola makubwa yanakiuka haki za nchi zinazoendelea kutokana na mtazamo wao wa kujifanyia mambo watakavyo na wa upande mmoja.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Feb 16, 2016 03:39 UTC
  • Balozi wa Iran UN akosoa siasa za upande mmoja za madola makubwa

Balozi na mwakilishi wa kudumu wa Iran katika Umoja wa Mataifa amesema madola makubwa yanakiuka haki za nchi zinazoendelea kutokana na mtazamo wao wa kujifanyia mambo watakavyo na wa upande mmoja.

Gholamali Khoshroo ambaye alikuwa akihutubia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwa niaba ya nchi wanachama wa Harakati ya Nchi Zisizofungamana na Siasa za Upande Wowote (NAM) amesema maadhimisho ya miaka 70 ya kuundwa kwa umoja huo ni fursa ya kuilinda Hati ya Umoja wa Mataifa ikiwa ndiyo njia pekee ya kudhamini amani na usalama duniani. Ameongeza kuwa kutojali nchi zilizoendelea haki za kiuchumi na kijamii za nchi zinazoendelea kumeitia hatarini amani na usalama wa dunia.

Balozi na mwakilishi wa kudumu wa Iran katika Umoja wa Mataifa ameongeza kuwa kwa mtazamo wa NAM, kuheshimu haki ya mamlaka ya utawala ya taifa, usawa kwa nchi zote, kujitawala na kupinga utumiaji mabavu na au vitisho katika uhusiano wa kimataifa ni usuli na mambo ya msingi ambayo yana ulazima wa kuheshimiwa na nchi zote.

Khoshroo amebainisha kuwa haipasi kuchukua hatua za upande mmoja za uadui wa kiuchumi dhidi ya mataifa kwa lengo la kubana uhuru na kujitawala kwa baadhi ya nchi wanachama wa Harakati ya Nchi Zisizofungamana na Siasa za Upande Wowote.

Aidha amesisitiza kwa mara nyengine juu ya msimamo wa NAM kwamba Hati ya Umoja wa Mataifa ina uwezo na njia kadhaa za kutatulia migogoro ya kimataifa; hivyo kuna ulazima wa kuzitumia zaidi fursa za sura ya sita na ya nane ya hati hiyo na kwamba utumiaji wa sura ya saba ikiwa ni njia ya mwisho ya utatuzi ufanyike pale tu amani na usalama wa kimataifa zunapokuwa zimekabiliwa na tishio kubwa na la kweli.../