Namna vita dhidi ya Iran vilivyobadilisha muundo wa soko la nishati duniani?
Taasisi moja ya Marekani imekiri kwamba vita dhidi ya Iran vimebadilisha pakubwa muundo wa soko la nishati duniani.
Taasisi hiyo kwa jina, Baraza la Atlantiki, imesema vita dhidi ya Iran na kuendelea kufungwa Lango-Bahari la Hormuz kumelitumbukiza soko la nishati duniani katika hali ya wasiwasi mkubwa, na matokeo yake ni makubwa kwa usalama wa nishati, biashara na sera za kiuchumi kaika ngazi za kimataifa. Kwa mujibu wa Baraza la Atlantiki, vita vya Asia Magharibi vimesababisha upungufu wa mapipa milioni 12 ya mafuta kila siku katika soko la kimataifa na kupunguza kwa kiasi kikubwa usambazaji wa gesi. Kutokana na hali hiyo, bei ya LNG barani Asia imeongezeka kwa asilimia 143.
Wakati huo huo, Umoja wa Afrika na Benki ya Maendeleo ya Afrika pia zimeonya kwamba ikiwa mzozo wa Asia Magharibi utachukua zaidi ya miezi 6, uchumi wa bara hilo utapoteza hadi asilimia 0.2 ya ukuaji wa Pato la Taifa mwaka 2026. Kwa maelezo hayo, kadiri mgogoro wa Asia Magharibi utakavyochukua muda mrefu kutatuliwa na mvutano kuongezeka kuhusu njia za meli na namna ya kudhamini usambazaji wa nishati na mbolea, kuna hatari ya kupungua pakubwa ukuaji wa uchumi katika bara zima la Afrika.
Wataalamu nchini Uingereza pia wameonya juu ya hatari ya kupungua chakula, huku bei ya nishati ikipanda na misururu ya usambazaji bidhaa ikitatizwa na vita vya kivamizi vinavyoendelea dhidi ya Iran. Wamewashauri raia kuweka akiba ya mahitaji muhimu yasiyoharibika haraka majumbani. Gazeti la Guardian limeandika hivi: Katika “ulimwengu wenye msukosuko,” lazima familia zijitayarishe kwa ajili ya kukatizwa ugavi wa chakula unaosababishwa na vita, mabadiliko ya hali ya hewa na hata mashambulizi ya mtandaoni.”