Qalibaf: Majenerali wa Marekani hawataki kufa kwa ajili ya Israel
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i137806-qalibaf_majenerali_wa_marekani_hawataki_kufa_kwa_ajili_ya_israel
Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu yaani Bunge la Iran, amekejeli hatua ya Waziri wa Vita wa Marekani, Pete Hegseth ya kuwatimua makamanda wenye uzoefu katika jeshi la nchi hiyo na kuandika: Hawataki tena kumtii mtangazaji wa televisheni anayehatarisha maisha ya Wamarekani kwa ajili ya njozi za Israel.
(last modified 2026-04-05T05:42:01+00:00 )
Apr 05, 2026 05:42 UTC
  • Mohammad Baqer Qalibaf, Spika wa Bunge la Iran
    Mohammad Baqer Qalibaf, Spika wa Bunge la Iran

Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu yaani Bunge la Iran, amekejeli hatua ya Waziri wa Vita wa Marekani, Pete Hegseth ya kuwatimua makamanda wenye uzoefu katika jeshi la nchi hiyo na kuandika: Hawataki tena kumtii mtangazaji wa televisheni anayehatarisha maisha ya Wamarekani kwa ajili ya njozi za Israel.

Kwa mujibu wa Fars News Mohammad Baqer Qalibaf, Spika wa Bunge la Iran, ameandika ujumbe kwenye akaunti yake ya mtandao wa kijamii wa X akisema: “Ripoti ya hali halisi: Majenerali wenye uzoefu wa jeshi la Marekani hawako tayari kuwa watu wa ‘ndiyo bwana’ kwa mtangazaji wa televisheni anayetaka kuifanya Marekani ijitoe kafara kwa ajili ya njozi za Israel.”

Qalibaf amesisitiza: “Hii ni gharama ya muda mfupi. Gharama ya muda mrefu itakuwaje? Walipakodi wa Marekani watalipia kwenye vituo vya mafuta kwa miongo kadhaa.

Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu ameongeza kuwa: Huu ndio urithi watakaoucha nyuma yao!”

Majuzi, Waziri wa Vita wa Marekani, Pete Hegseth, alimlazimisha Mkuu wa Majeshi ya nchi hiyo (Army Chief of Staff), Jenerali Randy George, kustaafu mara moja, huku kukiwa na mgogoro unaozidi kuongezeka ndani ya uongozi wa jeshi nchini humo kufuatia kushindwa vita vya nchi hiyo na Israel dhidi ya Iran.

Kutimuliwa ghafla mkuu huyo wa 41 wa majeshi ya Marekani kulifanyika Alhamisi iliyopita, katika kile kinachoonekana kuwa operesheni pana ya kuwapiga kalamu nyekundu makamanda waandamizi wa Marekani wasiokubaliana na vita haramu dhidi ya Iran.

Afisa mmoja wa Pentagon ameliambia gazeti la The Hill kuwa Hegseth mwenyewe alitoa amri kwa Jenerali George ajiuzulu na kustaafu mara moja.

Tangu kuingia madarakani, Hegseth, anayejulikana kuwa mwanajeshi Mkristo mwenye misimamo mikali, amewafukuza zaidi ya maafisa 12 wa ngazi za juu, akiwemo Naibu Mkuu wa Majeshi ya Anga Jenerali James Slife, mkuu wa Shirika la Ujasusi wa Kijeshi Luteni Jenerali Jeffrey Kruse, na Mkuu wa Operesheni za Jeshi la Wanamaji Adm. Lisa Franchetti.

 Wachambuzi wa masuala ya kijeshi wanaamini kuwa baadhi ya majenerali waliofutwa kazi walipinga vita dhidi ya Iran wakiamini kuwa Marekani haiwezi kuvishinda.