Ayatullah Khatami: Saudia ni chimbuko la magaidi wa Daesh (ISIS)
Khatibu wa Sala ya Ijumaa Tehran amesema jinai za kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh au ISIS zinatokana na fikra za kuwakufurisha Waislamu ambazo zinatawala Saudi Arabia.
Ayatullah Sayyed Ahmad Khatami ameashiria jina za ISIS katika Siku Kuu ya Idul Adha nchini Syria na kusema, ukatili wa ISIS unatokana na fikra za Kiwahabi ambazo chimbuko lake ni Saudi Arabia.
Ayatullah Khatami ameongeza kuwa, tokea ukoo wa Aal Saud uingie madarakani kwa msaada wa Uingereza huko Hijaz, ambayo sasa inaitwa Saudia, ukoo huo umekuwa ukijihusisha na mauaji na uporaji mali za Waislamu. Ameongeza kuwa, kile ambacho kinashuhudiwa leo nchini Yemen ni natija ya karne tatu za ukatili, unyakuzi na uporaji unaotekelezwa na ukoo wa Aal Saud.
Khatibu wa Sala ya Ijumaa Tehran amesema utawala wa Saudia ni utawala ulio dhidi ya haki za binaadamu na kuongeza kuwa, wakuu wa Saudia wamekuwa na uhusiano wa siri na utawala wa Kizayuni wa Israel, uhusiano ambao leo umebainika wazi na ungali unaendelea. Amesema Saudi Arabia ni mshirika wa jinai za Israel katika vita vyake dhidi ya wananchi madhulumu na wasio na ulinzi Palestina.

Ayatullah Khatami amesema ushirikiano wa Saudia na Israel ni doa katika historia ya ukoo wa Aal Saud. Aidha ametoa bishara kuwa, katika mustakabali wa karibu, ulimwengu wa Kiislamu utashuhudia kusambaratika ukoo huo.
Khatibu wa Sala ya Ijumaa Tehran pia ameashiria mapatano ya usitishwaji vita Syria na kusema Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inaunga hatua yoyote ambayo itapelekea kumaliza umwagaji damu Syria.
Ayatullah Khatami amesema Marekani na madola mengine ya Magharibi ni chanzo za kuendelea umwagaji damu Syria. Ameongeza kuwa njia pekee ya kumaliza mgogoro wa Syria ni Marekani kusitisha uungaji mkono wake kwa makundi ya kigaidi katika nchi hiyo.