Sep 17, 2016 09:16 UTC
  • Mahudhurio ya Iran katika Klabu ya Kimataifa ya Nyuklia

Mkuu wa Shirika la Nishati ya Atomiki la Iran (IAEO) Ali Akbar Salehi amehutubia kongamano la kila mwaka la Klabu ya Kimataifa ya Nyuklia mjini London, Uingereza akisisitzia udharura wa kuwepo ushirikiano katika masuala ya teknolojia ya nyuklia.

Salehi ametoa mapendekezo kadhaa katika kikao cha wataalamu cha kongamano hilo ambayo yamepongezwa na kukaribishwa na hadhirina. Mapendekezo hayo yanahusiana na jinsi ya kupanua zaidi utumiaji wa teknolojia ya nishati ya nyuklia na jinsi ya kutekeleza makubaliano ya nyuklia kati ya Iran na nchi za kundi la 5+1. 

Salehi amependekeza kuundwa kamati ya masuala ya ufundi kwa ajili ya kufanya tathmini kamili ya vituo vidogo vidogo vya nyuklia, kuchunguza masuala yote ya kiufundi, kiuchumi na kiusalama ya vituo hivyo na matokeo yake yakabidhiwe kwa nchi zinazoomba uanachama katika klabu hiyo. Mkuu wa Shirika la Nishati ya Atomiki ya Iran pia ametoa pendekezo la kuwepo ushirikiano kati ya vyuo vikuu vya Iran na Chuo Kikuu cha Klabu ya Kimataifa ya Nishati ya Nyuklia, suala ambalo limekaribishwa na kupongezwa katika mkutano wa London.

Suala jingine lililopendekezwa na Iran na kukubaliwa na Klabu ya Kimataifa ya Nyuklia ni kuundwa kamati maalumu ya kisiasa na kiufundi kwa ajili ya kuchunguza makubaliano ya nyuklia kati ya Iran na kundi la 5+1 kwa kifupi JCPOA. Salehi amesema kamati hiyo ambayo itakuwa taasisi isiyopendelea upande wowote, itachunguza utekelezaji wa makubaliano ya JCPOA, kiwango cha kushikamana na kuheshimiwa makubaliano hayo na pande husika na kutoa taarifa za mara kwa mara ili iweke wazi jinsi pande husika zinavyotekeleza makubaliano hayo.

Ali Akbar Salehi

Mapendekezo yaliyotolewa na Mkuu wa Shirika la Nishati ya Atomiki ya Iran katika kongamano la Klabu ya Kimataifa ya Nyuklia mjini London yanaonesha kuwa, Iran iko katika harakati kubwa yenye lengo la kustawisha zaidi ushirikiano wake na taasisi zinazojihusisha na elimu na teknolojia ya nyuklia. Kuwepo kwa Iran katika miradi ya kisasa kama ule wa nuclear fusion na ushirikiano wa Shirika la Nishati ya Atomiki la Iran na Klabu ya Kimataifa ya Nyuklia vyote ni kielelezo cha uwezo mkubwa wa Jamhuri ya Kiislamu katika teknolojia na elimu ya nyuklia. Mafanikio hayo sasa yamefikia kiwango cha kimataifa. 

Katika upande mwingine matamshi ya Mkuu wa Shirika la Nishati ya Atomiki la Iran katika kongamano la Klabu ya Kimataifa ya Nyuklia mjini London akisisitiza kuwa Wamagharibi hawajatekeleza ipasavyo makubaliano ya nyuklia kati ya Iran na kundi la 5+1 yanaakisi wasiwasi uliopo kwamba nchi za Magharibi zinatumia makubaliano ya JCPOA kama mwavuli wa kuhalalisha kusuasua kwao katika utekelezaji wa majukumu yao.

Salehi amesisitiza katika mazungumzo yake na gazeti la The Guardian la Uingereza kwamba, Iran imetekeleza kikamilifu majukumu yake kwa mujibu wa makubaliano ya kihistoria ya nyuklia ya JCPOA lakini licha ya kupita miezi 8 saa tangu kuondolewa vikwazo vulivyowekwa dhidi ya Iran, Magharibi bado haijatekeleza majukumu yake katika uwanja huo. Salehi amesisitiza kuwa pande mbili zinapaswa kutekeleza kikamilifu makubaliano hayo. 

Teknolojia ya nishati ya nyuklia ni haki ya taifa la Iran

Kuwepo kwa Iran katika Klabu ya Kimataifa ya Nyuklia kunaonesha maendeleo makubwa ya wasomi na wataalamu wa Jamhuri ya Kiislamu katika elimu ya nyuklia, suala ambalo halipaswi kufumbiwa jicho. Awali Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki ulikuwa ukikataa kushirikiana na Iran kwa kutumia visingizio visivyo na msingi lakini sasa kipindi hicho cha vikwazo kimepita na kutoweka.

Tags