Magaidi wawili raia wa Pakistan wakamatwa nchini Iran
Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (SEPAH) limetangaza habari ya kutiwa mbaroni raia wawili wa Pakistan katika mji wa Saravan wa mkoa wa Sistan va Baluchestan kwenye mpaka wa Iran na Pakistan.
Ofisi ya Mawasiliano ya Umma ya Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu imetangaza habari hiyo na kusema kuwa, magaidi hao wawili wametiwa mbaroni kwenye operesheni ya kushitukiza, kabla ya kufanya uhalifu wowote ule. Baada ya kutiwa mbaroni imegundulika kuwa magaidi hao ni raia wa Pakistan na ni wanachama wa genge moja la kigaidi linaloichukia Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Magaidi hao wameingia humu nchini kwa lengo la kufanya vitendo vya kigaidi.
Uchunguzi uliofanywa kwenye eneo walilokuwa wamefikia umepelekea kukamatwa mabomu ambayo yalikuwa yatumike kushambulia maeneo yenye watu wengi ndani ya ardhi ya Iran. Ofisi hiyo aidha imesema kuwa, kumepatikana siri nyingi katika usaili waliofanyiwa magaidi hao, na taarifa zake zitatangazwa katika siku za usoni.
Wakati huo huo siku ya Jumapili, Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu SEPAH lilifanikiwa kusambaratisha genge moja la magaidi tisa wa kundi la kigaidi linalojiita Jeyshul Adl, katika mkoa wa Sistan va Baluchistan. Jeshi la Sepah lilifanikiwa kumwangamiza kiongozi wa kigenge hicho na magaidi wengine watatu katika operesheni hiyo. Operesheni zote hizo zimefanyika kwenye maeneo ya mpaka wa Iran na Pakistan.
Magaidi wanaopata uungaji mkono wa madola ya kigeni wamekuwa wakifanya njama za mara kwa mara za kujipenyeza kwenye mipaka ya Iran ili kuendesha vitendo vya kihalifu, hata hivyo njama zao nyingi zinashindwa kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu, kwa kuwa macho askari wa kulinda usalama wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kwa ushirikiano kamili wa wananchi.