Rais Rouhani: Utendaji wa Marekani ni kinyume cha mapatano ya nyuklia
Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema, tume ya pamoja ya kuratibu mapatano ya nyuklia, maarufu kama Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezaji (JCPOA), imesema utendaji wa Marekani ni kinyume cha mapatano hayo.
Rais Rouhani ameyasema hayo leo asubuhi alipowasilia katika Uwanja wa Ndege wa Mehrabad mjini Tehran baada ya kumaliza safari yake ya Venezuela, Cuba na kisha New York kwa ajili ya kushiriki katika kikao cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa. Akibainisha mafanikio ya safari hiyo ya wiki moja, Rais Rouhani amesema Marekani sasa imeahidi kurekebisha msimamo wake kuhusu utekelezwaji wa mapatano hayo.
Makubaliano hayo ya nyuklia yalifikiwa Julai 14 mwaka jana mjini Vienna nchini Austria kati ya Iran na Kundi la 5+1, na kuanza kutekelezwa Januari mwaka huu. Hata hivyo Marekani imekuwa ikiweka vizingiti katika utekelelzwaji wake.
Rais Rouhani pia ameashiria safari yake nchini Venezuela kwa ajili ya kushiriki katika mkutano wa Jumuiya ya Nchi Zisizofungamana na Siasa za Upande Wowote NAM ambapo alimkabidhi Rais wa Venezuela, Nicolás Maduro, uenyekiti wa harakati hiyo. Amesema akiwa katika mkutano huo alikutana na kufanaya mazungumzo na marais wa nchi nane.
Kuhusu safari yake nchini Cuba, Rais Rouhani amesema alikutana na Fidel Castro, Kiongozi wa Mapinduzi ya Cuba na pia rais wa nchi hiyo Raul Castro.
Akiwa New York, Rais Rouhani mbali na kuhutubu katika kikao cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa pia alikutana na viongozi wa nchi mbali mbali kama vile Uingereza, Ufaransa, Italia, Japan, Ugiriki, Pakistan, Iraq na pia Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon.