Iran inalenga kuimarisha zaidi uhusiano na nchi za Afrika
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema, kuimarisha uhusiano na nchi za Kiafrika ni msingi muhimu wa sera za kigeni za Iran.
Rais Hassan Rouhani ameyasema hayo leo hapa mjini Tehran alipokutana na kufanya mazungumzo na Abdullah Mabri Waziri wa Mambo ya Nje wa Ivory Coast na kuongeza kuwa amefurahishwa na mkondo wa ustawi wa uhusiano wa nchi hizi mbili. Rais Rouani amesisitiza kuwa, Iran iko tayari kuimarisha uhusiano wake na Ivory Coast katika nyanja zote hasa katika sekta za kiuchumi.
Rais Rouhani amesema Iran imeweza kustawi katika sekta mbali mbali kama vile za kiufundi na kiuhandisi na kuongeza kuwa, Iran inaweza kuisaidia Kodivaa katika ujenzi wa barabara na miradi ya kuzalisha umeme.
Akigusia kadhia ya ugaidi, Rais wa Iran amesema, kuna haja ya nchi zote kushirikiana katika kukabiliana na tatizo hilo. Amesema ugaidi ni tatizo kubwa katika dunia na kwamba magaidi hawana uhusiano wowote na Uislamu kwani Uislamu ni dini ya kupendana, amani na kuishi pamoja kwa amani na kwamba, dini hii inapinga vitendo vyote vya ghasia na ukatili.
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameongeza kuwa, Wairani 17,000 wameuawa shahidi kutokana na ugaidi na hivyo nchi hii imepata hasara kubwa katika vita dhidi ya ugaidi. Ameongeza kuwa Iran itazisaidia nchi zote zinazotaka kupambana na ugaidi.
Kwa upande wake, Abdullah Mabri, Waziri wa Mambo ya Nje wa Ivory Coast ameishukuru Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa msaada wake kwa nchi yake. Aidha amesema, nchi yake inataka kuimarisha uhusiano na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika nyanja zote hasa za kiuchumi.