Nov 13, 2016 16:08 UTC
  • Iran yalaani hujuma ya kigaidi nchini Pakistan

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imelaani shambulio la kigaidi lililotokea jana Jumamosi katika mkoa wa Baluchestan nchini Pakistan, ambapo makumi ya watu waliuawa na wengine wengi kujeruhiwa.

Bahram Qassemi, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje wa Iran sanjari na kutoa mkono wa pole kwa waathirika wa hujuma hiyo ya kigaidi, amesema juhudi za pamoja zinahitajika ili kung'oa mizizi ya ugaidi duniani. Amesema akthari ya waliouawa katika shambulio hilo la Pakistan ni wanawake na watoto na hivyo juhudi za dhati zinahitajika ili kulikabili jinamizi la ugaidi duniani.

Hujuma ya kigaidi Pakistan

Huku hayo yakiarifiwa, idadi ya waliouawa katika hujuma hiyo ya kinyama mkoani Baluchestan imeongezeka na kufikia watu 52 kutoka idadi ya awali ya 47.

Hapo jana kundi la kigaidi la Daesh lilishambulia kwa bomu Haram ya Shah Noorani katika wilaya ya Lasbela, mkoa wa Baluchestan, kusini magharibi mwa Pakistan. Watu 500 walikuwa kwenye Haram hiyo wakati wa hujuma hiyo ya kigaidi.

Itakumbukwa kuwa, makurutu zaidi ya 50 pia waliuawa baada ya magaidi ya Daesh kushambulia chuo cha kutoa mafunzo ya polisi katika mji wa Quetta, kusini magharibi mwa Pakistan.

Tags