Mamilioni ya Wairani wamejitokeza kupiga kura
(last modified Fri, 26 Feb 2016 16:18:36 GMT )
Feb 26, 2016 16:18 UTC
  • Mamilioni ya Wairani wamejitokeza kupiga kura

Mamillioni ya wananchi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran wamejitokeza kupiga kura katika chaguzi mbili muhimu Ijumaa hii.

Wairani wamepiga kura katika uchaguzi Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge) yenye wajumbe 290 na uchaguzi Baraza la Wanazuoni Wataalamu Wanaomchagua Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu lenye wajumbe 88. Kutokana na idadi kubwa ya wapiga kura, zoezi la upigaji kura, ambalo lilianza saa mbili asubuhi na kupangwa kumalizika saa 12 jioni kwa saa za Iran, limerefushwa kwa masaa kadhaa katika maeneo mbali mbali nchini.

Maafisa wa ngazi za juu wa Iran akiwemo Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Khamenei, Rais Hassan Rouhani, Spika wa Bunge Ali Larijani na maulamaa wa ngazi za juu walipiga kura mapema Ijumaa asubuhi na kutoa wito kwa wananchi kujitokeza kwa wingi, wito ambao umeitikiwa kwa kishindo.

Wairani milioni 55, wametimiza masharti ya kupiga kura huku kukiwa na masanduku 129,000 ya kupigia kura ambayo yamewekwa kwenye vituo 53,000 vya kupigia kura kote Iran. Aidha zaidi ya maafisa nusu milioni wamesimamia zoezi la uchaguzi mwaka huu. Matokeo ya uchaguzi yatatangazwa katika kipindi cha siku chache zijazo.

Kuna wagombea 4,844, wakiwemo wanawake 500 wanaowania viti vya bunge huku kukiwa na wagombea 161 wanaowania nafasi katika Baraza la Wanazuoni Wataalamu. Chaguzi huru na za haki hufanyika mara kwa mara nchini Iran kwa kuhudhuriwa na mamilioni ya wananchi.

Tags