"Obama atasaini mpango wa kurefusha vikwazo dhidi ya Iran"
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i20635
Baada ya Seneti ya Marekani kupitisha mpango wa kurefusha vikwazo dhidi ya Iran, afisa mmoja mwandamizi katika Ikulu ya Marekani (White House) amesema Rais wa nchi hiyo Barack Obama anatazamiwa kusaini mpango huo na kuwa sheria.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Dec 03, 2016 04:24 UTC

Baada ya Seneti ya Marekani kupitisha mpango wa kurefusha vikwazo dhidi ya Iran, afisa mmoja mwandamizi katika Ikulu ya Marekani (White House) amesema Rais wa nchi hiyo Barack Obama anatazamiwa kusaini mpango huo na kuwa sheria.

Afisa huyo wa serikali ya Marekani amekieleza kituo kimoja cha habari kuwa Obama atautia saini mpango huo wa kurefusha vikwazo dhidi ya Iran katika kipindi cha siku 10 zijazo.

Hii ni katika hali ambayo Rais wa Marekani hapo kabla alikuwa akisisitiza kila mara kwamba ataupigia kura ya veto mpango wowote utakaohatarisha na kukiuka makubaliano ya nyuklia yaliyofikiwa baina ya madola makuu sita duniani na Iran.

Ikulu ya Marekani, White House

Afisa huyo mwandamizi katika Ikulu ya Marekani ameongeza kuwa serikali ya Washington inaitakidi kuwa Kongresi na Seneti za nchi hiyo hazijakiuka makubaliano ya nyuklia na Iran; kwa hiyo hakuna sababu ya kumzuia Rais Obama kusaini mpango huo wa kurefusha vikwazo dhidi ya Iran kwa kipindi kingine cha miaka 10.

Marekani ni moja ya nchi sita zilizosaini makubaliano ya nyuklia ya Iran (JCPOA) ambayo yameitaka Iran ipunguze na kusimamisha baadhi ya shughuli zake za nyuklia mkabala na kuondolewa vikwazo vyote vya kimataifa na vya upande mmoja ilivyowekewa kwa sababu ya shughuli zake hizo.

Iran na nchi za kundi la 5+1 ziliposaini makubaliano ya JCPOA

Viongozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran wameshasisitiza mara kadhaa kuwa kurefushwa vikwazo dhidi ya taifa hili ni ukiukaji wa makubaliano ya nyuklia ambao lazima utakabiliwa na jibu na radiamali ya Iran.../