Zarif: Kurefusha vikwazo kunaonesha kuwa serikali ya Marekani haina muamana
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i20656-zarif_kurefusha_vikwazo_kunaonesha_kuwa_serikali_ya_marekani_haina_muamana
Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema, kwa mtazamo wa jamii ya kimataifa kurefushwa vikwazo vya Marekani dhidi ya Iran kunaonesha kuwa serikali ya Washington haina muamana.
(last modified 2026-03-03T12:46:59+00:00 )
Dec 03, 2016 04:23 UTC
  • Zarif: Kurefusha vikwazo kunaonesha kuwa serikali ya Marekani haina muamana

Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema, kwa mtazamo wa jamii ya kimataifa kurefushwa vikwazo vya Marekani dhidi ya Iran kunaonesha kuwa serikali ya Washington haina muamana.

Muhammad Javad Zarif ameyasema hayo mbele ya waandishi wa habari mapema leo mara baada ya kuwasili New Delhi, mji mkuu wa India likiwa ni jibu na radiamali yake kwa hatua ya kurefushwa vikwazo vya Marekani dhidi ya Iran.  Zarif amesisitiza kuwa inachofanya Marekani ni kinyume na ahadi inazowajibika kutekeleza kulingana na makubaliano ya nyuklia (JCPOA). 

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amefafanua kuwa hata kama hatua iliyochukuliwa na Kongresi ya Marekani dhidi ya Iran itapitishwa kwa kusainiwa na Rais wa nchi hiyo Barack Obama haitokuwa na athari ya kiutekelezaji.

Wakati huohuo Ali Akbar Salehi, Mkuu wa Shirika la Nishati ya Atomiki la Iran amesema mpango uliopitishwa na Seneti ya Marekani wa kurefusha vikwazo vya miaka 10 dhidi ya Iran ni ukiukaji wa wazi wa makubaliano ya nyuklia (JCPOA).

Ali Akbar Salehi, Mkuu wa Shirika la Nishati ya Atomiki la Iran

Mkuu wa Shirika la Nishati ya Atomiki la Iran amesisitiza kuwa hatua za lazima ambazo Iran itachukua kukabiliana na uamuzi wa Baraza la Wawakilishi na Seneti ya Marekani zitatangazwa kwa wakati wake baada ya maamuzi yatakayopitishwa na viongozi waandamizi.

Siku ya Alkhamisi Seneti ya Marekani ilipitisha kwa kura 99 za wajumbe waliounga mkono bila ya kupingwa na mjumbe yeyote mpango wa kurefusha kwa miaka 10 mingine sheria ya vikwazo dhidi ya Iran. Kabla ya hapo Baraza la Wawakilishi la Marekani liliupitisha mpango huo kwa kura 419 za kuunga mkono dhidi ya kura moja tu iliyoupinga.

Mpango huo wa vikwazo unaolenga kuchukua hatua dhidi ya sekta za benki, nishati na ulinzi za Iran unasubiri kusainiwa na Rais wa nchi hiyo Barack Obama ili uwe sheria.../