Dec 12, 2016 07:22 UTC
  • Iran yalaani hujuma ya kigaidi dhidi ya eneo la kidini Misri

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amelaani shambulizi la kigaidi lililolenga kanisa moja katika mji mkuu wa Misri, Cairo na kusababisha vifo vya makumi ya watu.

Bahram Qassemi, amesema kuhujumiwa maeneo matukufu ya kidini ni kinyume kabisa na mafundisho ya dini yeyote ile huku akitoa wito wa kuimarishwa ushirikiano miongoni mwa dini na nchi mbali mbali duniani kwa shabaha ya kulikabili jinamizi la ugaidi.

Hapo jana watu wasiopungua 25 waliuawa na wengine zaidi ya 50 kujeruhiwa katika shambulizi hilo la bomu, katika kanisa la Wakristo wa Kikhufti (Coptic), katika mji mkuu Cairo.

Inaarifiwa kuwa, bomu hilo liliripuka pambizoni mwa kiti cha Papa wa Wakristo wa Kikhufti, anayeongoza jamii ya Wakrsito walio wachache nchini Misri.

Shughuli za uokoaji nje ya kanisa la Kikhufti jijini Cairo

Bahram Qassemi, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ameongeza kuwa, shambulizi hilo dhidi ya kanisa tena wakati huu ambapo wafuasi wa dini hiyo wanakaribia kuadhimisha Krismasi (kumbukubu ya kuzaliwa Nabii Issa AS) ni kitendo cha kioga, kinachodhihirisha kwa mara nyingine tena kuwa ugaidi hautambui mipaka, utaifa wala imani.

Hapo jana Sheikh Ahmad al-Tayyib, Mkuu wa Chuo Kikuu cha Kiislamu cha Azhar cha Misri alilaani shambulizi hilo na kusisitiza kuwa, hujuma hiyo ya kigaidi ni jinai kuu dhidi ya Wamisri wote.

Rais Abdul Fattah al-Sisi wa Misri

Wakati huo huo, Rais Abdul Fattah al-Sisi wa Misri amelaani hujuma hiyo aliyoitaja kuwa ya kigaidi na kusema kuwa, vitendo hivyo vya kigaidi havina nafasi katika nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika.

Kadhalika maelfu ya wananchi wa Misri jana Jumapili waliingia mabarabarani mjini Cairo kufanya maandamano ya kulaani ukatili huo wa magaidi huku wakiitaka serikali ya Sisi ijiuzulu kwa kushindwa kuwadhaminia usalama wananchi.

Tags