Rais Rouhani amlaki rasmi Rais wa Indonesia
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amemlaki rasmi Rais wa Indonesia katika Ikulu ya Saad Abad hapa Tehran.
Rais Joko Widodo wa Indonesia leo asubuhi amelakiwa rasmi na Rais Hassan Rouhani wa Iran na kisha akakagua gwaride la heshima baada ya kupigwa nyimbo za taifa za nchi mbili hizi. Katika marasimu hayo, Rais wa Indonesia pia aliuarifisha ujumbe wa maafisa wa ngazi ya juu wa nchi yake aliofuatana nao ziarani hapa nchini.
Rais Hassan Rouhani na mwenzake wa Indonesia Joko Widodo wamefanya mazungumzo ya pande mbili baada ya marasimu hayo. Kuimarisha ushirikiano wa pamoja katika nyanja mbalimbali kati ya Iran na Indonesia kieneo na kimataifa; na vile vile kuimarishwa uhusiano kati ya Tehran na Jakarta katika nyanja mbalimbali ni moja ya masuala yaliyojadiliwa katika mazungumzo ya marais hao. Rais wa Indonesia jana aliwasili Tehran akiongoza ujumbe wa ngazi ya juu wa nchi hiyo kwa shabaha ya kufanya mazungumzo na viongozi wa ngazi ya juu wa Iran.