Marekani yarefusha vikwazo vya miaka kumi dhidi ya Iran
Katika kuendeleza uhasama na uadui wake dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, rasimu ya kurefusha vikwazo vya miaka kumi vya Marekani dhidi ya Iran imepasishwa na kuwa sheria bila ya kutiwa saini na Rais wa nchi hiyo.
Rais Barack Obama wa Marekani leo Alkhamisi hakutia saini rasimu ya kurefusha vikwazo vya miaka kumi dhidi ya Iran lakini muswada huo wa Kongresi ya nchi hiyo umebadikia la kuwa sheria moja kwa moja. Obama hakusaini muswada huo lakini ameruhusu uwe sheria bila ya kuutia saini.
Sheria hiyo ambayo inaweka msingi wa vikwazo vya upande mmoja vya Marekani dhidi ya Iran, ilipasishwa kwa mara ya kwanza mwaka 1996 kwa shabaha ya kuzuia uwekezaji mkubwa wa kigeni katika sekta ya mafuta na gesi nchini Iran na tangu wakati huo ilirefushwa tena mwaka 2006 kwa kipindi kingine cha miaka kumi. Muda wa sheria hiyo ulikuwa unamalizika mwishoni mwa mwaka huu wa 2016.
Baada ya kutiwa saini makubaliano ya nyuklia kati ya Iran na kundi la 5+1 ikiwemo Marekani, Rais Barack Obama alitoa amri ya kusitishwa vikwazo vya nchi hiyo vinavyohusiana na suala la nyuklia.
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inasisitiza kuwa, kurefushwa vikwazo vya Marekani dhidi ya Iran ni sawa na kuweka vikwazo vipya na kwamba huo ni ukiukaji wa makubliano ya nyuklia JCPOA yaliyobarikiwa na jamii ya kimataifa.