Dec 25, 2016 03:51 UTC
  • Firouzabadi: Uwahabi; adui wa umoja wa nchi za Kiislamu

Mshauri Mkuu wa kijeshi wa Amirijeshi Mkuu wa vikosi vya ulinzi vya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, uwahabi ambao matunda yake ni makundi ya kigaidi kama vile Daesh na al Qaida, ni maadui wa umoja na uhuru wa nchi za Kiislamu.

Shirika la habari la IRNA limemnukuu Meja Jenerali Hassan Firouzabadi akisema hayo na kusisitiza kuwa, mataifa ya Waislamu na hususan vijana wa nchi za Kiislamu leo hii wanapaswa kuwa macho zaidi kuliko wakati mwingine wowote na wasikubali kutekwa na njama za Wawahabi na makundi ya Daesh na al Qaida, wakafanya vitendo vilivyo kinyume na malengo makuu na matukufu ya Bwana Mtume Muhammad SAW.

Meja Jenerali Firouzabadi ameongeza kuwa, magaidi wa makundi ya Jabhatun Nusra na Ahrarush Sham ambao wamefanya jinai kubwa dhidi ya wananchi madhlumu wa Syria, hawana tofauti yoyote na magaidi wa Daesh isipokuwa majina tu ndiyo yanayotofautiana.

Kundi la kigaidi la Daesh

 

Vile vile amesema, mtandao wa al Qaida nao ni kama Daesh, hakuna tofauti yoyote baina ya makundi hayo mawili, kwani kundi hilo la al Qaida lilianzishwa nchini Afghanistan miaka kadhaa iliyopita, baadaye baadhi ya wanachama wa al Qaida walitoka kwenye kundi hilo na kwenda kuunda kundi la Daesh katika nchi za Iraq na Syria.

Meja Jenerali Firouzabadi pia amesema, makundi yanayowakufurisha Waislamu wengine ni vibaraka wa mabeberu na Uzayuni wa kimataifa. Hivyo Waislamu duniani wanapaswa kupata funzo kutokana na hali mbaya zilizoko katika nchi za Afghanistan, Iraq, Libya, Syria na Yemen na kuungana na kujiweka mbali na fikra za kukufurishana. 

Tags