Jan 13, 2017 03:40 UTC
  • Marais wa Iran na Uturuki wasisitiza udharura wa kupambana na ugaidi

Marais wa Iran na Uturuki wamesisitiza tena udharura wa kuimarishwa ushirikiano wa Tehran, Ankara na Moscow katika kuimarisha amani ya Mashariki ya Kati na kupambana na ugaidi.

Kauli hiyo imetolewa katika mazungumzo ya simu ya Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu na mwenzake wa Uturuki, Recep Tayyip Erdoğan aliyepiga simu kuwasilisha rambirambi za serikali yake na taifa la Uturuki kwa serikali na taifa la Iran kutokana na kifo cha Ayatulllah Hashemi Rafsanjani, aliyekuwa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Kuainisha Maslahi ya Mfumo wa Kiislamu. 

Katika mazungumzo hayo Dakta Rouhani pia ametoa mkono wa pole kwa Rais wa Uturuki kutokana na mauaji ya raia kadhaa wa Uturuki kwenye mashambulizi ya kigaidi ya hivi karibuni nchini humo na kusema kuwa, nchi hizi mbili zinaweza kushirikiana zaidi kwa ajili ya kung'oa mizizi ya ugaidi. 

Makundi ya kigaidi kama Daesh sasa yamewageuka hata mabwana zao na kuanza kuwang'ata

Rais Rouhani ameongeza kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inakaribisha ushirikiano wa karibu na mkubwa zaidi baina ya Tehran, Ankara na Moscow kwa ajili ya kuimarisha amani na usalama wa eneo la Mashariki ya Kati.

Kwa upande wake Rais Recep Tayyip Erdoğan wa Uturuki amesema kuwa nchi hizi mbili zina majukumu mazito katika eneo la Mashariki ya Kati na zinawajibika kuimarisha zaidi ushirikiano kwa ajili ya kuangamiza makundi ya kigaidi na kupunguza mivutano baina ya nchi za eneo hilo. 

 

Tags