Iran yalaani maamuzi ya Rais wa Marekani
Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imetoa taarifa na kulaani vikali uamuzi wa serikali ya Marekani wa kuzuia Waislamu kuingia nchini humo ikisema kuwa, huko ni kuuvunjia heshima waziwazi ulimwengu wa Kiislamu na taifa la Iran.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ilitoa taarifa hiyo jana na kusema kuwa, Uamuzi wa serikali ya Marekani wa kuwazuia Waislamu kuingia nchini humo, licha ya kudaiwa kuwa umechukuliwa kwa lengo la kukabiliana na ugaidi na kulinda usalama wa wananchi wa Marekani, lakini kwa hakika ni zawadi kwa makundi yenye misimamo mikali katika eneo la Mashariki ya Kati.
Katika taarifa yake hiyo, Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imesema: Wakati jamii ya kimataifa ikiwa inahitajia mazungumzo na kuchukuliwa hatua za kimsingi za kukabiliana na misimamo mikali na katika hali ambayo Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa limekubaliana na pendekezo la Iran la kushiriki mataifa yote ya dunia katika vita dhidi ya ugaidi na machafuko, serikali ya Marekani imeamua kuchukua hatua zisizo za kimantiki na kufanya ubaguzi wa wazi dhidi ya raia wa nchi za Kiislamu, suala ambalo bila ya shaka litatumiwa vibaya na makundi yenye misimamo mikali kueneza machafuko duniani.
Taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imeongeza kuwa, uamuzi huo wa Marekani unawalenga moja kwa moja wananchi wa Iran na kitendo hicho ni kulivunjia heshima taifa hili na wakati huo huo ni kudhihirisha dhati ya kiadui ya Marekani dhidi ya wananchi wa Iran, licha ya kwamba huko nyuma viongozi wa Marekani walikuwa wakijifanya kuwa hawana chuki na wananchi wa Iran.