Rais Rouhani ampokea rasmi Waziri Mkuu wa Sweden
Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran muda mchache uliopita amempokea rasmi katika ikulu ya Saad Abad mjini Tehran Stefan Löfven Waziri Mkuu wa Sweden aliyekuja hapa nchini kwa safari rasmi ya kikazi.
Baada ya mapokezi hayo rasmi yaliyoambatana na kupigwa nyimbo mbili za taifa za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Sweden viongozi hao walianza mazungumzo yao rasmi.
Taarifa zaidi zinasema kuwa, miongoni mwa mambo yatakayojadiliwa na Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Waziri Mkuu wa Sweden ni kupanuliwa ushirikiano wa pande mbili katika uga wa kiuchumi na kisiasa.
Aidha viongozi hao wanatarajiwa kuzungumzia matukio ya kieneo na kimataifa ikiwemo kadhia ya mgogoro wa Syria.
Stefan Löfven Waziri Mkuu wa Sweden aliwasili jana usiku hapa mjini Tehran akiuongoza ujumbe wa ngazi za juu wa kibiashara na kisiasa akiitikia mwaliko wa rasmi wa Rais wa Iran.
Akiwa hapa nchini, Stefan Löfven Waziri Mkuu wa Sweden mbali na Rais Rouhani, anatarajiwa pia kufanya mazungumzo na viongozi wengine wa ngazi za juu wa Tehran.