Balozi wa Palestina Tehran: Tunaishukuru sana Iran kwa kuiunga mkono Paletina
Balozi wa Palestina mjini Tehran sambamba na kuashiria umuhimu wa mkutano wa 6 wa kimataifa kwa ajili ya kuunga mkono Intifadha ya Palestina uliofanyika hapa mjini Tehran Jumanne na jana Jumatano, ambao uliionyesha dunia dhulma na ukatili wanaofanyiwa Wapalestina, amesema kuwa mkutano huo ulikuwa muhimu sana katika kufichua njama chafu za Marekani na utawala haramu wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Palestina.
Salah al-Zawawi ameyasema hayo katika mahojiano na Shirika la Habari la IRNA ambapo pamoja na mambo mengine ameshukuru sana misaada ya kila hali ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa Palestina kukiwemo kuanzisha mawasiliano imara baina ya nchi za Kiislamu kwa ajili ya kutiliwa umuhimu kadhia ya Palestina.
Al-Zawawi amesema kuwa, njama za kuhamisha ubalozi wa Marekani kutoka Tel Aviv kwenda Quds, kupanuliwa ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kiyahudi na kadhalika uporaji zaidi wa ardhi za Wapalestina na marufuku ya kuzuia adhana iliyotolewa na Israel huko katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu, yote hayo ni njama za Marekani. Ameongeza kuwa, uadui wa Marekani hususan wa Rais Donald Trump na Wazayuni dhidi ya Waislamu duniani unazidi kudhihirika kila siku.
Balozi wa Palestina mjini Tehran amefafanua umuhimu wa kuundwa taifa huru la Palestina mji mkuu wake ukiwa Quds na kwamba kufanyika mkutano huo wa kimataifa wa kuunga mkono Intifadha ya Palestina ni fursa adhimu kwa ajili ya kuondolewa vizingiti vya kufikiwa suala hilo. Kadhalika Salah al-Zawawi ameitaja Intifadha ya Tatu ya Wapalestina kuwa ni ishara ya kushindwa kwingine utawala haramu wa Kizayuni wa Israel na kwamba kupitia mashahidi kutaweza kufikiwa malengo ya mwisho.
Hayo yanajiri katika hali ambayo mkutano wa wanaharakati wanaounga mkono Palestina umefanyika leo hapa hapa mjini Tehran ikiwa ni siku moja baada ya kumalizika mkutano wa sita wa kimataifa wa kuunga mkono Intifadha ya Palestina uliofanyika hapa Tehran na kuwaleta pamoja washiriki zaidi ya 700 kutoka nchi 80 duniani.