Kongresi ya Marekani yajiandaa kuibana zaidi Iran kwa vikwazo vipya
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i26788-kongresi_ya_marekani_yajiandaa_kuibana_zaidi_iran_kwa_vikwazo_vipya
Maseneta wa Bunge la Kongresi la Marekani wameandaa muswada wa sheria inayopania kuiongezea vikwazo Jamhuri ya Kiislamu ya Iran eti kwa kufanyia majaribio makombora yake ya balistiki.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Mar 24, 2017 02:50 UTC
  • Kongresi ya Marekani yajiandaa kuibana zaidi Iran kwa vikwazo vipya

Maseneta wa Bunge la Kongresi la Marekani wameandaa muswada wa sheria inayopania kuiongezea vikwazo Jamhuri ya Kiislamu ya Iran eti kwa kufanyia majaribio makombora yake ya balistiki.

Maseneta 14 wa vyama vya Republican na Democrat jana Alkhamisi waliwasilisha katika Kongresi ya Marekani muswada huo, wakilalamikia hatua ya Iran kufanyia majaribio makombora yake ya balistiki na shughuli nyingine zisizokuwa za mradi wa nyuklia wa Tehran.

Hata hivyo, Robert Menendez, Seneta wa Jimbo la New Jersey wa chama wa Democrat amedai kuwa, muswada huo haukinzani na makubaliano ya nyuklia kati ya Iran na kundi la 5+1.

Kongresi ya Marekani ilitazamiwa kupasisha muswada huo wa kuibana zaidi Iran ya Kiislamu kiuchumi, kabla ya kongamano la lobi ya Kizayuni ya Kamati ya Marekani na Israel ya Masuala ya Umma AIPAC litakaloanza Jumapili ijayo.

Iran ikifanyia majaribio kombora la balestiki la Khorramshahr

Mwezi uliopita, Wizara ya Hazina ya Marekani ilitoa taarifa inayojumuisha asasi na shakhsia 25 katika orodha ya vikwazo vipya vya Marekani dhidi ya Iran, kwa kisingizio cha kufanya majaribio ya makombora.

Makubaliano ya nyuklia ambayo yanafahamika kwa kifupi kama JCPOA na ambayo yalifikiwa Julai 14 mwaka 2016 na kuanza kutekelezwa Januari mwaka jana kati ya Iran na madola sita makubwa duniani katika kundi la 5+1, yalitazamiwa kufungua ukurasa mpya katika uhusiano wa kisiasa na kiuchumi kati ya Tehran na nchi za Magharibi.

Hata hivyo, kama ilivyotarajiwa, Marekani imekuwa ikiweka vizingiti na kukiuka ahadi ilizotoa katika utekelezwaji wa mapatano hayo. Hii ni katika hali ambayo, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imekuwa ikisisitiza kuwa, vikwazo dhidi ya taifa hili havijawa na natija iliyodhamiriwa.