Marais wa Iran na Russia wasisitiza kustawishwa uhusiano wa nchi mbili
(last modified Tue, 28 Mar 2017 16:41:43 GMT )
Mar 28, 2017 16:41 UTC
  • Marais wa Iran na Russia wasisitiza kustawishwa uhusiano wa nchi mbili

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema katika mazungumzo na mwenzake wa Russia kuwa lengo la Iran na Russia ni kuimarisha amani na utulivu katika eneo.

Katika mazungumzo yake na Rais Vladimir Putin wa Russia yaliyofanyika mjini Moscow leo, Rais Rouhani ameongeza kuwa ushirikiano wa Tehran na Moscow hauilengi nchi nyengine yoyote ile ya tatu.

Dakta Rouhani ameashiria mwenendo wa ustawi wa ushirikiano kati ya Iran na Russia katika miaka ya karibuni na kueleza kwamba: Tehran na Moscow zimepata tajiriba na uzoefu mzuri katika kupambana na ugaidi wa kimataifa na magendo ya biashara haramu ya mihadarati.

Marais wa Iran na Russia katika mazungumzo mjini Moscow

Rais wa Iran aidha amesema ana matumaini kwamba katika mazungumzo ya pande mbili zitapigwa hatua mpya katika kustawisha ushusiano wa Tehran na Moscow.

Kwa upande wake, Rais Vladimir Putin wa Russia amesema Iran ni jirani mwema na mshirika thabiti na wa uhakika wa nchi yake na kubainisha kuwa Russia na Iran zina uhusiano wa miaka mingi; na kwa upande wa kidiplomasia, uhusiano wao unapindukia zaidi ya miaka 500.

Putin amesisitiza kuwa Russia na Iran zinashirikiana katika nyanja zote ikiwemo masuala ya kimataifa, utatuzi wa masuala magumu mno katika uga huo pamoja na kadhia za kiuchumi.

Rais Rouhani na mwenyeji wake Rais Putin katika mazungumzo na waandishi wa habari

Rais wa Russia ameashiria pia kuongezeka kwa asilimia 70 mabadilishano ya kibiashara baina ya nchi mbili katika mwaka uliomalizika wa 2016 kulinganisha na mwaka 2015 na kueleza kwamba mafanikio hayo yamepatikana katika hali tata ya kiuchumi inayotawala hivi sasa.

Ripoti kutoka Moscow zinaeleza kuwa baada ya mazungumzo ya marais wa nchi mbili, zimesainiwa hati 14 za ushirikiano baina ya Iran na Russia katika sekta mbalimbali ikiwemo ya masuala ya viza, utalii, uchumi, mawasiliano, sheria na vyombo vya mahakama.

Rais Hassan Rouhani aliwasili mjini Moscow hapo jana akiongoza ujumbe wa ngazi ya juu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa safari rasmi nchini humo.../