Meja Jenerali Baqeri: Iran haitetereshwi na vita vya kisaikolojia vya Marekani
Mkuu wa Vikosi vya Ulinzi vya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema taifa hili halibabaishwi na vita vya kisaikolojia vya Marekani na waitifaki wake.
Katika mkutano na makamanda, wakurugenzi na maafisa wa ngazi za juu wa Jeshi la Iran jana Jumanne hapa mjini Tehran, Meja Jenerali Muhammad Hossein Baqeri alisema Iran imeweza kusimama kidete na kujihami vyema na kivitendo mkabala wa uvamizi na vitisho vyovyote vya maadui na hivyo haitiwi kiwewe na propaganda na vita vya kisaikolojia vya Marekani.
Mkuu wa Vikosi vya Ulinzi vya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesisitiza kuwa, Kujihami Kutakatifu kwa taifa la Iran ni jambo ambalo linapaswa kuwa na mazingatio kwa watu ambao daima wanaiendea mbio nchi hii ili kuidhuru huku akisisitiza kuwa, Jeshi la Iran litaendelea kuimarisha uwezo wa kujihami, kutokana na taifa hili kuzungukwa na vitisho vingi.
Ameongeza kuwa wataalamu wa kijeshi wa Iran wana uwezo wa hali ya juu katika kukidhi mahitaji ya kiulinzi ya taifa hili.
Kadhalika ameashiria namna vyombo vya usalama vya Iran ya Kiislamu vimefanikiwa kuzima njama za magenge ya kigaidi ambayo yamekuwa yakijaribu kujipenyeza nchini na kuvuruga usalama wa taifa.
Meja Jenerali Muhammad Hossein Baqeri amesema ushirikiano mzuri wa Jeshi la Iran na Idara ya Intelijensia, umesaidia kutibulia njama nyingi za mashambulizi ya kigaidi hapa nchini licha ya makundi hayo ya kitakfiri kupata uungaji mkono na ufadhili kutoka madola ya kibeberu.