Apr 10, 2017 07:36 UTC
  • Iran yalaani mashambulizi ya kigaidi dhidi ya Makanisa Misri

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imelaani vikali mashambulizi ya kigaidi dhidi ya makanisa mawili nchini Misri hapo jana, ambapo makumi ya watu waliuawa na wengine wengi kujeruhiwa.

Bahram Qassemi, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje wa Iran sambamba na kutoa mkono wa pole kwa familia za wahanga, serikali na taifa la Misri kwa ujumla kufuatia hujuma hizo za kikatili, amesema mashambulizi dhidi ya maeneo ya ibada, matukufu ya kidini na dhidi ya mikusanyiko wa watu wasio na hatia na ulinzi, ni jambo lisilokubalika.

Amesisitiza kuwa, harakati za kigaidi duniani zinaweza kuzimwa tu kwa ushirikiano na mashauriano ya serikali za eneo na kimataifa akibainisha kuwa, vita dhidi ya magenge ya kigaidi haviwezi kufanikiwa bila mshikamano.

Kanisa la Kikhufti lililoshambuliwa na magaidi Misri

Hii ni katika hali ambayo, Harakati ya Kiislamu ya Hizbullah ya nchini Lebanon na ile ya Palestina HAMAS  zimelaani vikali hujuma hizo za magaidi wa kundi la kitakfiri la Daesh, zilizosababisha watu karibu 140 kuuawa na kujeruhiwa nchini Misri.

Magaidi waliwalenga kwa mabomu Wakristo ambao jana walikuwa wanaadhimisha Jumapili ya Matawi, katika Kanisa la Kikhufti (Coptic) mjini Tanta na kanisa jingine katika mji wa Alexandria, eneo la Nile Delta. 

Tags