Kampeni za uchaguzi wa rais Iran zaanza
Baada ya mkuu wa Tume ya Uchaguzi ya Iran, kutangaza majina ya wagombea sita wa uchaguzi wa 12 wa Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, kampeni zimeanza rasmi leo Ijumaa.
Ali Asghar Ahmadi amesema kwa mujibu wa kifungu cha 66 cha sheria ya uchaguzi ya Iran, kampeni za uchaguzi huanza siku wanapotajwa rasmi wagombea waliotimiza masharti ya kugombea urais humu nchini.
Alkhamisi usiku, Baraza la Kulinda Katiba ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, liliwasilisha kwa Wizara ya Mambo ya Ndani majina ya wagombea sita waliotimiza masharti ya kugombea urais.
Wagombea sita walioidhinishwa kugombea urais ni pamoja na Sayyid Mostafa Aqa-Mirsalim, Sayyid Mostafa Hashemi-Taba, Es'haq Jahangiri, Mohammad-Baqer Qalibaf, Seyyed Ebrahim Raeisi na Hassan Rouhani.
Kwa mujibu wa sheria ya uchaguzi ya Iran, kampeni za wagombea urais zinaanza tangu siku walipotangazwa rasmi wagombea hadi masaa 24 kabla ya kuanza zoezi la upigaji kura. Uchaguzi wa 12 wa Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran unatarajiwa kufanyika Ijumaa ya tarehe 19 mwezi ujao wa Mei sambamba na uchaguzi wa tano wa mabaraza ya Kiislamu ya miji na vijiji kote nchini Iran.
Mbali na uchaguzi wa rais pia kutafanyika uchaguzi wa mabaraza ya Kiislamu ya miji na vijiji na pia uchaguzi mdogo wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu yaani Bunge la Iran.