Waafghani: Iran ndio inafanya juhudi kubwa kurejesha amani nchini kwetu
Licha ya Marekani na washirika wake katika eneo kueneza propaganda chafu dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran wachambuzi wa masuala ya kisiasa nchini Afghanistan, wamekaribisha na kupongeza juhudi za taifa hili kwa ajili ya kudumisha usalama na amani nchini mwao na nafasi ya Tehran katika uwanja huo.
Weledi hao wa masuala ya kisiasa nchini Afghanistan, wameisifia safari ya hivi karibuni ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Mohammad Javad Zarif nchini humo na kuongeza kuwa, safari hiyo ni yenye umuhimu katika kipindi hiki muhimu.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, safari ya Zarif mjini Kabul imetajwa kuwa itasaidia katika kustawisha ushirikiano wa nchi mbili. Ghulam Mohammed, mchambuzi wa masuala ya kisiasa wa Afghanistan, amezungumza na Redio Tehran na kusema kuwa, Waafghanistan wanaamini kwamba, Tehran ina nafasi chanya katika kuupatia ufumbuzi mgogoro wa nchi za eneo ikiwemo Afghanistan. Ameongeza kuwa, njia pekee ya kuiondoa Afghanistan katika mgogoro wa sasa ni kuimarisha ushirikiano na nchi majirani hususan Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Sami'i mchambuzi mwengine wa masuala ya kisiasa wa nchini Afghanistan amesema kuwa, kupatikana usalama nchini humo kutategemea na usalama wa nchi majirani zake.
Ameongeza kuwa, Afghanistan ina matumaini ya kupata msaada katika uga wa kupambana na ugaidi kutoka nchi majirani hususan Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.