Iran: Lengo la Marekani ni kuudhoofisha ulimwengu wa Kiislamu
Mkuu wa Kamati ya Usalama wa Taifa ya Bunge la Iran amesema, lengo la Marekani ni kuudhoofisha ulimwengu wa Kiislamu, kushadidisha mizozo katika eneo hili, kuuza silaha nyingi zaidi na kuweka kambi nyingi zaidi za kijeshi katika nchi kama vile Saudi Arabia.
Shirika la habari la IRIB limemnukuu Alaeddin Boroujerdi akisema hayo leo wakati alipohojiwa na kanali ya tatu ya televisheni ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuhusiana na safari ya Rais wa Marekani Donald Trump nchini Saudi Arabia na kuongeza kuwa, kitendo cha nchi hizo mbili cha kutiliana saini mkataba wa dola bilioni 110 kinaonesha kuwa, Marekani itazidi kufyonza mafuta ya Saudi Arabia katika mkabala wa kuiuzia silaha nchi hiyo, silaha ambazo hivi sasa zinatumika kuulia kwa umati watu wasio na hatia wa Yemen kwa baraka kamili za Marekani. Jumla ya mikataba iliyotiwa saini baina ya tawala hizo mbili ina thamani ya dola bilioni 380 za Marekani.
Amesema, kitendo cha nchi kadhaa za Kiislamu cha kumkaribisha rais wa Marekani huko Saudi Arabia ni ukurasa mwingine mweusi katika historia ya umma wa Kiislamu.
Aidha amesema, Marekani na Saudi Arabia ndio waliopata pigo katika matukio ya Iraq, Syria na Afghanistan na kwamba Saudia ndiyo sehemu kunakozaliwa fikra za kundi la kigaidi la Daesh na leo hii Marekani na Saudi Arabia zinaliunga mkono kundi hilo ingawa kidhahiri zinajifanya kulipinga.
Rais wa Marekani Donald Trump aliwasili nchini Saudi Arabia ikiwa ni safari yake ya kwanza ya nje ya Marekani tangu alipotangazwa kuwa rais wa nchi hiyo. Katika ziara hiyo, Marekani imewekeana na Saudi Arabia mikataba mingi ya kuiuzia silaha, biashara na uchumi.