Iran na New Zealand kustawisha ushirikiano
Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Iran na New Zealand wamesisitizia umuhimu wa kuimarisha uhusiano wa pande mbili haswa katika uga wa kiuchumi.
Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran, Muhammad Javad Zarif ambaye aliwasili New Zealand hapo jana amezungumza na kubadilishana mawazo na mwenzake Murray McCully wa nchi hiyo juu ya kustawisha uhusiano wa nchi mbili hizi katika nyuga tofauti za kiuchumi na vilevile juu ya masuala ya kieneo. Zarif amesema Tehran iko tayari kupiga hatua kubwa na kupanua uhusiano wake na Wellington katika nyuga zote. Kwa upande wake Murray McCully, Waziri wa Mambo ya Nje wa New Zealand amepongeza juhudi za Iran katika kujaribu kuipatia ufumbuzi migogoro inayolikumba eneo la Mashariki ya Kati.
Zarif kadhaika amekutana na kufanya mazungumzo na Wairani wanaoishi na kufanya kazi nchini New Zeland, na kuwataka watumie fursa zilizopo haswa baada ya makubaliano nyuklia ya Iran maarufu kama JCPOA.
Kabla ya kuitembelea New Zealand, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran alikuwa amezitembelea Thailand, Indonesia, Singapore na Brunei. Muhammad Javad Zarif anatazamiwa kuelekea Australia katika duru ya mwisho ya safari yake ya nchi 6 za bara Asia na Pacific.