Brig. Jenerali Jazayeri: Marekani, Saudia ni waongozaji wa ugaidi wa Daesh
Msemaji wa Majeshi ya Iran amesema Marekani na Saudi Arabia ndio waongozaji na waungaji mkono wakuu wa kundi la kigaidi la ISIS au Daesh.
Brigedia Jenerali Massoud Jazayeri ambaye pia ni Naibu wa Kamandi Kuu ya Majeshi ya Iran amesema: "Kundi la ISIS linafungamana na Marekani na Saudi Arabia na linatekeleza hujuma kwa muongozo na uungaji mkono wa nchi hizo mbili."
Ameongeza kuwa, "leo tunashuhudia matokeo haribifu ya ugaidi wa kiserikali unaoungwa mkono na Marekani na Saudia kwa ushirikiano wa baadhi ya madola ya kieneo." Ametaja mfano wa natija ya ugaidi huo kuwa ni hali ya Iraq, Syria, Afghanistan, Yemen na nchi kadhaa za Ulaya."
Karibu watu 17 waliuawa shahidi na wengine 50 kujeruhiwa Juni saba wakati magaidi walipotekeleza hujuma za pamoja katika Bunge la Iran na Haram Takataifu ya Imam Khomeini MA mjini Tehran.
Kundi la kigaidi la ISIS lilitangaza kuhusika na hujuma hizo.
Brigedia Jenerali Jazayeri amesema watu wa Iran wana nguvu na tokea mwanzo wa ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu hadi sasa wameshuhudia hujuma kadhaa za kigaidi na hivyo wanaweza kukabiliana na uhasama wa adui pasina kuondoka katika mkondo wao wa haki na kwa wataendeleza mapambano yao dhidi ya ugaidi.