Kiongozi: Kupambana na utawala wa Kizayuni ni kupambana na ubeberu na uistikbari
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i30786-kiongozi_kupambana_na_utawala_wa_kizayuni_ni_kupambana_na_ubeberu_na_uistikbari
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameitaja Siku ya Kimataifa ya Quds kuwa yenye umuhimu mkubwa na kuongeza kuwa: "Siku hii mbali na kuwa ni siku ya kuunga mkono taifa lililodhulumiwa pia ni nembo ya kupambana na uistikbari na ubeberu duniani."
(last modified 2026-02-22T02:21:18+00:00 )
Jun 22, 2017 03:36 UTC
  • Kiongozi: Kupambana na utawala wa Kizayuni ni kupambana na ubeberu na uistikbari

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameitaja Siku ya Kimataifa ya Quds kuwa yenye umuhimu mkubwa na kuongeza kuwa: "Siku hii mbali na kuwa ni siku ya kuunga mkono taifa lililodhulumiwa pia ni nembo ya kupambana na uistikbari na ubeberu duniani."

Ayatullah Sayyed Ali Khamenei Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu aliyasema hayo Jumatano alasiri mjini Tehran alipokutana na wahadhiri, watafiti na wasomi wa vyuo vikuu vya Iran. Akiashiria Siku ya Kimataifa ya Quds inayoadhimishwa Ijumaa, Kiongozi Muadhamu aliongeza kuwa: "Kuadhimisha Siku ya Quds hakumaanishi tu kutetea taifa  lililodhulumiwa na kutimuliwa kutoka nyumba zao, bali leo kutetea Palestina ni kutetea ukweli ambao ni zaidi ya kadhia ya Palestina."

Ameendelea kusema kuwa: "Kupambana na utawala wa Kizayuni ni kupambana na mfumo wa kibeberu na ni kwa sababu hii ndio watawala wa Marekani wakawa na uhasama na harakati hii na wakawa wanahisi inawapa pigo."

Aidha Kiongozi Muadhamu katika hotuba yake ameashiria jukumu na kazi ya ualimu na uhadhiri na kusema: "Mhadiri ambaye ana fikra chanya, anawajibika, ana matumanaini na anazingatia masuala ya kidini, kitaifa na kimapinduzi huku akiwa na azma imara anaweza kuwa na nafasi katika kumuwezesha mwanachuo atafakari na kuwa na nafasi ya kipekee.

Mkutano wa Kiongozi Muadhamu na wahadhiri

Ayatullah Khamenei amesema madola ya kibeberu yamekuwa na njama ya kujaribu kuzuia kuingia sayansi mpya katika vyuo vikuu vya Iran ili kuvidhoofisha. Ameongeza kuwa katika zama za utawala wa wafalme wa Kipahlavi, Wamagharibi hawakuvipa vyuo vikuu vya Iran uwezo muhimu wa sayansi na teknolojia mpya na badala yake walivibadilisha vyuo vikuu kuwa sehemu ya kupenyeza thamani za Kimagharibu huku wakizuia ubunifu katika vyuo hivyo.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuokoa vyuo vikuu kutoka katika mkondo potovu, kudiriki umuhimu wa sayansi na teknolojia na kuibua harakati katika vyuo vikuu ni  kati ya baraka za Mapinduzi ya Kiislamu. Aidha amesema idadi kubwa ya wanachuo ambao wameinukia katika mazingira hayo sasa ni wahadhiri ambao  wanainua viwango vya vyuo vikuu nchini huku wakilinda thamani za Kiislamu na za Mapinduzi ya Kiislamu.