Jun 30, 2017 14:00 UTC
  • Rais Rouhani aipongeza  Iraq kwa kuwatimua magaidi wa ISIS kutoka Mosul

Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameipongeza Iraq kufuatia mafanikio ya kukombolewa mji wa Mosul ambao ulikuwa unakaliwa kwa mabavu na kundi la kigaidi la ISIS au Daesh.

Katika ujumbe wake kwa Rais Fouad Masoum wa Iraq, Rais Rouhani amesema kuangamizwa kundi la kuogofya la ISIS ni  ushindi dhidi ya ugaidi na misimamo mikali na ushindi huo umetokana na jitihada zisizo na kikomo za jeshi na vikosi vya kujitolea vya wananchi nchini humo pamoja na msaada wa nchi jirani.

Aidha katika ujumbe mwingine kwa Waziri Mkuu wa Iraq Haider al Abadi, Rais Rouhani amesema ushindi huu mkubwa ulipatikana kutokana na ushirikiano, kujitolea muhanga na jitihada za watu waliopata masaibu na vikosi shujaa vya kujitolea vya wananchi vya Hashd al Shaabi,  pamoja na ushirikiano wa nchi jirani. Amesema ushindi dhidi ya ISISI huko Mosul umeonyesha mapambano ya kweli dhidi ya magaidi ambao wamekuwa wakiwaua watu kidhulma kwa jina la Uislamu.

Wanajeshi wa Iraq wakisherehekea ushindi Mosul

Rais Rouhani amesema Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inajiunga na watu wa Iraq katika furaha yao kufuatia kukombolewa mji wa Mosul na kwamba  iko tayari kuendelea kusaidia katika vita dhidi ya ugaidi katika eneo. Rais wa Iran pia amemtumia pia ujumbe Ayatullah Sistani, Marjaa wa Waislamu wa Madhehebu ya Shia nchini Iraq  na kusema: "Ushindi wa watu wa Iraq na kukombolewa mji wa Mosul, kwa mara nyingine kumewawekea wazi walimwengu nafasi na hadhi ya juu ya ''Umarjaiya na Fatwa."

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema miaka mitatu iliyopita, wakati wa siku zilizojaa vurugu na misukosuko, ni vyuo vya kidini na marajii ndio walioleta matumaini na kuonyesha irada ya kukabiliana na ugaidi na hivyo kuwawezesha wananchi na jeshi kukabiliana na wavamizi.

Jana Alhamisi televisheni ya Iraq ilitangaza kukomblewa mji wa Mosul na hivyo kuangamizwa rasmi kundi la kigaidi la ISIS ambalo lilikuwa limejitangazia dola lake nchini humo.

Tags